Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano TRA, Bw. Richard Kayombo akizungumza leo Oktoba 25, 2023 Mkoani Morogoro wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wakuu wa vitengo vya Mawasiliano na Masoko wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha mjini Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha Bw. Benny Mwaipaja akifafanua jambo wakati wa kongamano hilo liliofanyika mjini Morogoro.
Benny Mwang’onda Mwenyekiti wa wahariri katika Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wakuu wa vitengo vya Mawasiliano na Masoko wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha
…………………………….
NA JOHN BUKUKU, MOROGORO.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejipanga kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa sheria mbalimbali ili waweze kukusanya mapato pamoja na kuishauri serikali kuhusu masuala ya sera za mapato ya Taifa.
Akizungumza leo Oktoba 25, 2023 Mkoani Morogoro wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wakuu wa vitengo vya Mawasiliano na Masoko wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha lenye lengo la kujengeana uwelewa kwenye masuala la habari, masoko na mawasiliano, Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano TRA, Bw. Richard Kayombo amesema kuwa lengo ni kuinua kiwango cha ulipaji wa kodi kwa hiyari kwa watanzania.
Bw. Kayombo amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya ulipaji wa kodi kutokana na kukosekana kwa mazingira rafiki ambayo yatasaidia wafanyakazi kulipa kwa wakati na kufuata utaratibu.
“Malengo yetu tuwawezesha watanzania kulipa kodi pamoja na kuendelea kutoa elimu kuwa lini anapaswa kulipa na wakati gani na namna gani anaweza kulipa” amesema Bw. Kayombo.
Amesema kuwa pia watahakikisha wanadhibiti aina zote za udanganyifu pamoja na ukwepaji wa kodi kwani kumekuwa na baadhi ya watu hawalipi au kulipa kidogo tofauti na uhalisia.
Bw. Kayombo amesema kuwa TRA ni taasisi ya umma ambayo inagusa kila Idara katika utekelezaji wa majukumu yake na kuhakikisha wanafikia malengo husika.
Amesema kuwa pia wanawajibika kulinda mikataba ya nchi ili kuhakikisha vitu haviingii bila kufuata utaratibu na sheria za nchi.
Amebainisha kuwa makusanyo ya kodi yamekuwa yakiongezeka kutokana na uhitaji wa serikali kwa ajili kutoa huduma kwa wananchi wake.
“Kila mwaka bajeti ya serikali inapanda kutoka mahitaji yanaongezeka katika maeneo mbalimbali, na wanategemea vyanzo vya mapato ikiwemo kodi” amesema Bw. Kayombo.