Kamisaa wa sensa Taifa ,Anna Makinda akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo mkoani Arusha.
Waandishi wa habari kutoka kanda ya kaskazini wakisikiliza semina hiyo iliyofanyika mkoani Arusha .
……………………
Julieth Laizer ,Arusha .
Arusha .Mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela amewataka waandishi wa habari kanda ya kaskazini kuripoti taarifa zenye takwimu sahihi kwa maslahi ya wananchi kwani wao ndio wanaotegemewa na jamii kwa kiwango kikubwa.
Ameyasema hayo mkoani Arusha wakati akifungua mafunzo ya wanachama wa vyama vya waandishi wa habari wa mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Manyara kuhusu usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanayofanyika mkoani Arusha na kuandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimua.
Amesema kuwa,waandishi wa habari wana wajibu mkubwa sana katika kuhabarisha wananchi kuhusu taarifa mbalimbali na ni wajibu wao kuhakikisha taarifa hizo zinakuwa sahihi ili kusaidia jamii.
Mongela amesema utoaji wa takwimu sahihi wakati wa kuripoti taarifa mbalimbali katika jamii utasaidia sana wananchi kupata taarifa zinazoeleweka na zenye uhakika zaidi.
“unajua nyie waandishi wa habari ndo mna majukumu ya kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na za uhakika kwani jamii inawategemea kwa kiwango kikubwa kikubwa sana hivyo nawaombeni sana mhakikishe mnakuwa wa kweli wakati wa kuripoti taarifa zenu.”amesema.
Kwa upande wa Kamisaa wa sensa Taifa Anna Makinda amesema waandishi wa habari wamefanya kazi kubwa tena kwa utulivu katika kipindi cha sensa ambapo amesema takwimu zetu sasa zinahalalika kiulimwengu na elimu inayotolewa haina kikomo kwani takwimu ni hali haisikiki katika nchi yetu.
Amesema ni lazima waandishi wa habari wahakikishe wanashirikiana kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na halisi katika jamii .
“Nawashauri msifanye kazi hiyo kwa hofu kwani mkifanya kwa hofu kazi hazitaenda vizuri hivyo naombeni mtumie nafasi zenu vizuri kuelimisha jamii na waweze kupata uelewa mzuri pia.”amesema Makinda.
Amesema kuwa, ni lazima turudishe matokeo ya sensa kwa wenyewe waliohesabiwa ili waweze kupata maendeleo endelevu kwa maslahi ya nchi yetu kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi NBS,Dk Amina Msengwa amewataka waandishi wa habari waliopata fursa ya mafunzo hayo kutumia elimu waliyopata kuwaelimisha wananchi kwa kutoa taarifa sahihi ili wananchi wahabarike na kupata taarifa zenye ukweli.
Aidha kauli mbiu ya sensa ni “matokeo ya sensa ya sita mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu”.