Na Sophia Kingimali
Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA) limewataka wasimamizi wa mtihani ya upimaji wa darasa la nne na kidato cha pili kuwa waadilifu na weledi kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi apate haki yake.
Jumla ya wanafunzi 1,692,802 wa darasa la nne wamesajiliwa kufanya upimaji huo ambapo kati yao Wavulana 828,591 sawa na asilimia 48.95 na wasichana 864,211 sawa na asilimia 51.05.
Hayo ameyasema leo Oktoba 24 Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bw. Said Mohamed wakati akitoa taarifa rasmi ya kuanza upimaji wa mitihani hiyo ambapo upimaji wa darasa la nne unaanza Oktoba 25 na 26 na kidato cha pili oktoba 30 mpaka novemba 9.
Amesema maandalizi yote kwa ajili ya upimaji huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo katika Halmashauri na manispaa zote nchini.
“Maandalizi yote yamekamilika na watahiniwa wenye mahitaji maalum yamefanyika ipasavyo na kamati za mikoa na halmashauri zimefanya semina ili kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya upimaji yapo salama,utulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu”amesema Mohamed.
Aidha katibu huyo amewataka wamiliki na wakuu wa Shule kutambua kuwa Shule zao ni vituo maalum vya mtihani hivyo hawatakiwi kwa namna yeyote kuingilia majukumu ya wasimamizi.
Pia amewataka wananchi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha upimaji wa mitihani hiyo unafanyoka katika utulivu na amani.
Waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha pili ni wanafunzi 759,573 ambao wamesajiliwa ambao kati yao wavulana 353,807 sawa na asilimia 46.58 na wasichana 405,766 sawa na asilimia 53.42 ambapo wanafunzi wenye mahitaji maalum wapo 1,382 kati yao 683 ni wenye uoni hafifu,82 ni wasioona,290 wenye ulemavu wa kusikia na 309 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili na 18 wenye ulemavu wa akili.