Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Mhandisi Shafi Shaban kushoto,akijibu malalamiko ya wakazi wa kijiji cha Isale wilayani humo kuhusiana na kuchelewa kwa ujenzi wa mradi wa maji ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2017 na Halmashauri ya wilaya Nkasi.
Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Mhandisi Shafi Shaban wa pili kulia na Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa uwasa mkoa wa Rukwa Mhadisi Davis Lameck wa kwanza kushoto, wakikagua mradi wa kulaza mabomba kwenye mradi wa maji wa Isale wilayani Nkasi ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 75,kulia diwani wa kata ya Nduchi Franzis Mkoswe.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Isale wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa,wakiwa na meneja wa Ruwasa wilayani humo Mhandisi Shafi Shaban ambapo walimuomba kusimamia kwa karibu mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Isale kukamilisha ujenzi wake ili waweze kuondokana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama.
Na Muhidin Amri,
Nkasi
BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Isale kata ya Isale wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa,wamemuomba mkandarasi anayejenga mradi wa maji katika kijiji hicho kukamilisha haraka ujenzi huo ili waweze kuondokana na adha ya kutumia maji ya visima ambayo siyo safi na salama.
Walisema, mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2017 lakini hadi sasa bado haujakamilika na wanaendelea kuteseka kwa kutembea umbali mrefu na kutumia maji ya visima vya asili yanayopatikana mbali na makazi yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Peter Bukuku alisema, kila siku wananchi wa kijiji hicho wanaamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwa matumizi yao,hali inayopelekea kusuasua kwa shughuli mbalimbali za maendeleo kijijini hapo.
Ameikumbusha serikali,kutimiza ahadi ya kukamilisha mradi huo ili na wao waanze kutumia maji ya bomba kama ilivyo kwenye maeneo mengine hapa nchini kwa sababu ni muda mrefu tangu mradi huo ulipoanza kutekelezwa kupitia Halmashauri ya wilaya Nkasi.
Paul Kifunda alisema,kuchelewa kwa mradi huo kumepelekea baadhi ya miundombinu yake ikiwemo tenki la kuhifadhi maji lililojengwa katika kijiji hicho kuchakaa kabla ya kuanza kutoa huduma huku baadhi ya vijana wanalitumia kuvutia bangi na kufanya uharifu mwingine.
Jema Damson alisema,kero ya maji katika kijiji hicho imesababisha ndoa nyingi kuvunjika hasa pale akina mama wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao familia zao.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Nkasi Mhandisi Shafi Shaban alisema,Ruwasa imepokea mradi huo mwaka 2019 kutoka Halmashauri ya wilaya na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 75.
Alisema,mradi wa maji Isale unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 5.5 na wamepokea Sh.bilioni 2.8 na utakapokamilika utahudumia jumla ya kata tatu zenye vijiji sita vya Isale A na B,Nduchi,Ifundwa,Kitosi,Msilihofu na Nkata zenye jumla ya wakazi 35,000.
Alitaja kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa mateki sita ya ukubwa tofauti,ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 42,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 76 na ujenzi wa chanzo cha maji na kazi zilizobaki ni ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 32 kati ya kilomita 42.
Aidha alitaja sababu za kutokamilika mradi huo kwa wakati ni kutokana na kuchelewa kwa fedha za kumlipa mkandarasi kiasi cha Sh.milioni 850.
Hata hivyo alisema,wanatarajia kupokea fedha kutoka serikalini ambazo zitalipwa kwa mkandarasi ili aweze kukamilisha mradi huo na wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.