Tanzania imethibitishwa na Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) kuwa Mjumbe wa Baraza Tendaji la Shirika hilo kwa kuchaguliwa bila kupingwa na nchi wanachama wa Shirika la UNWTO.
Uchaguzi huo umefanyika tarehe 19 Oktoba, 2023 Jijini Samarkand, Uzbekistan ambako Mkutano Mkuu wa 25 wa UNWTO unaendelea.
Kupitia nafasi hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb) ataiwakilisha Afrika kwa kipindi cha Miaka minne (2023 – 2027) katika mikutano muhimu ya Baraza hilo itayokuwa ikifanyika mara mbili (2) kwa mwaka.
Akizungumza baada ya Tanzania kuthibitishwa katika nafasi hiyo, Mhe. Kairuki ameeleza kuwa nafasi hiyo ni muhimu katika kukuza na kutangaza utalii wa Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuwa Baraza hilo ni chombo muhimu kinacho simamia Mipango na Bajeti ya Shirika pamoja na utekelezaji wake.
Aidha, Mhe. Waziri ameongeza kuwa, kupitia nafasi hii, Tanzania itashiriki kupeleka agenda muhimu zenye maslahi mapana ya maendeleo ya utalii wa Bara la Afrika.