Waziri wa katiba na sheria balozi Pindi Chana akizungumza na waandishi wa habari juu ya kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaotarajiwa kuanza kesho octoba 20 hadi Novemba 9, 2023 jijini Arusha.
………………………
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha. Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya haki za binadamu na watu ambapo watajadili mada mbalimbali juu ya haki za binadamu na watu Afrika.
Aidha Kikao hicho cha siku 20, kinahusisha sekta mbalimbali ya masuala ya haki za binadamu na watu, ambapo pia watajadili Maadhimisho ya siku ya haki za binadamu Afrika kwa kuzingatia itifaki ya maputo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo , Waziri wa katiba na sheria balozi Pindi Chana amesema kuwa maandalizi yote ya mkutano huo yamekamilika na utakuwa na washiriki zaidi ya 1300 wakiwemo wajumbe 700.
“Katika mkutano huo utakaofunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dr. Mwinyi utajadili pia taarifa kuhusu haki za binadamu Afrika, na uzinduzi wa nyaraka mbalimbali za kamisheni ya Afrika ya haki za binadamu na watu” alisema Chana.
“Mbali na hilo pia kutakuwa na taarifa ya shughuli mbali mbali za wajumbe wa kamisheni, za wanaharakati wa haki za binadamu na watu pia kuidhinisha kwa itifaki wa mkataba wa Afrika wa ulinzi wa jamii”
Waziri Chana, aliwataka wananchi kuwa wakarimu kipindi chote cha mkutano huo, ikiwemo kudumisha Amani na utulivu lakini zaidi kuchangamkia fursa mbali mbali ikiwemo utoaji huduma kwa wageni katika manufaa ya kiuchumi.
“Naombeni tutumie mkutano huu kama fursa kwani Tanzania tunatarajia kuitumia kuitangaza nchi kimataifa hasa vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji na kuzifanya nchi hizi kutamani kuja kujifunza”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Ephraim Mafuru amesema kuwa jumla ya wageni 1300 wamejiandikisha wakiwemo 919 kutoka nje ya nchi.