Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi, Lucas Kambelenje akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Shirika la Ndege Nchini (ATCL) hawapo pichani, wakati alipofungua Kikao cha tano cha Baraza hilo linalofanyika mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi akitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje (kulia) kuhusu utendaji wa shirika kabla ya ufunguzi wa kikao cha tano cha Baraza hilo linalofanyika mkoani Morogoro.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje (hayupo pichani), wakati alipofungua Kikao cha tano cha Baraza hilo, Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje (wa pili kulia waliokaa), katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL) mara baaada ya kufungua kikao cha tano cha baraza hilo, mkoani Morogoro.PICHA NA WIZARA YA UCHUKUZI.
……………
ATCL YATAKIWA KUPATA FAIDASerikali imelitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuhakikisha linapanga mikakati madhubuti itakayoliwezewesha kukua na kujiendesha kwa tija baada ya uwekezaji mkubwa unaofanywa kupitia ununuzi wa ndege za masafa mafupi, ya kati na marefu.
Akizungumza wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Pili la Wafanyakazi mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema ununuzi wa ndege hizo unaofanywa pamoja na maboresho katika viwanja unatarajiwa kuongeza tija katika usafiri wa anga nchini.
“Kama Serikali tunategemea ndege hizi 14 zilizonunuliwa ziwe na matokeo chanya ambayo yataonekana na niwahakikishie kuwa ndege zilizobaki Serikali itahakikisha zinakuja ili Shirika liendelee kupiga hatua”, amesema Kambelenje.
Mkurugenzi Kambelenje ameipongeza ATCL kwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwawezesha wataalam wa kampuni hiyo kufanya matengenezo ya ndege wenyewe kwa matengenezo makubwa (C Check) hapa nchini hali inayookoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingelipwa kwa makampuni ya nje ya nchi.
Aidha, Kambelenje ameitaka ATCL kuhakikisha inaboresha huduma kwa wateja ili kuvutia wateja wengi zaidi kutumia Shirika hilo kwa safari za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imeweza kutengeneza mifumo mbalimbali ya tehama inayotumika kwenye mauzo ya tiketi pamoja kuingia makubaliano na mashirika mengine ya kimataifa ili kupata wateja kwenye maeneo ambayo ATCL haitoi huduma.
Mkurugenzi Matindi amebainisha kwamba, ATCL imefanikiwa kuongeza vituo vya safari kutoka vine (4) hadi kufikia vituo 15 vya ndani na 11 vya nje ya nchi.
Baraza la Wafanyakazi wa ATCL linakutana kwa siku mbili mkoani Morogoro ambapo pamoja na kufanya tathimini ya utendaji Shirika hili pia litajadili Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano (Corporate Strategic Plan 2022/23 – 2026/27) wa Kampuni hiyo. (Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Uchukuzi).