Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo tarehe 17 octoba, 2023 amezindua matumizi rasmi ya gari maalumu la kubebea wagonjwa lilitengenezwa na wataamu kutoka idara ya uhandisi hospitalini hapa imetengeneza gari maalum la kubebea wagonjwa wasio na uwezo wa kutembea wanaokuja kupatiwa matibabu hospitalini hapa.
Akiongea kwenye hafla hiyo ya kuanza matumizi ya gari la kubebea wagonjwa, Dkt. Godlove Mbwanji Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amesema ubunifu wa gari hilo maalumu utaenda kupunguza changamoto kwa watoa huduma ambao hapo awali walikuwa wakitumia viti mwendo pamoja na vitanda vya matairi kupeleka wagonjwa maeneo mbalimbali ya kutolea huduma hospitani ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
“..gari hili inaenda kuchukua nafasi ya vile viti mwendo na vitanda vya matairi hivyo kusaidia kutokuwa na kazi ya kutumia nguvu wakati wa kuwabeba wagonjwa na hivyo kuwasababishia wengi shida za migongo, napenda kumshukuru Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan na Wizara Afya inayoongozwa na Mhe Ummy Mwalimu kwa mchango wa kuunga mkono huduma mbalimbali za afya zinazotolewa hapa hospitali pamoja na ubunifu unaofanywa na wataalam wa Sekta ya Afya katika kuboresha huduma za afya nchini.” – Dr. Mbwanji
Dkt. Mbwanji ameipongeza Idara ya Uhandisi Hospitalini kwa bunifu mbalimbali zinazofanywa ikiwemo za mfumo wa kumpa taarifa mtoa huduma pindi mgonjwa anapo hitaji msaada pamoja na mfumo wa kurekebisha hali joto katika chumba cha watoto wachanga kilichopo katika idara ya huduma ya afya ya mzazi na watoto wachanga META.
Fredrick Ndondole ni Mtaalamu kutoka idara ya Uhandisi amesema wazo hilo lilitoka kwa Uongozi wa hospitali na kulichakata na wao kitengo cha uhandisi wakalichukua na kulichakata na kuunda gari ambalo litaweza kubeba mgonjwa na mtoa huduma kutoka eneo moja la kutolea huduma kwenda eneo jingine la kutolea huduma hivyo kuja na wazo ambalo ni Rafiki kwa mazingira ya hospitali na linatumia umeme.
“..tulipokea wazo kutoka kwa Mkurugenzi wa hospitali kutokana na changamoto iliyokuwa ikiwapata watumishi kutokana na kusukuma wagonjwa kwa mikono kwa kutumia viti mwendo na vitanda vya matairi..”
Alta Mpogole, muuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ameushukuru Uongozi wa Hospitalini hapo na kusema uwepo gari hilo maalumu la kubeba wagonjwa litakuwa msaada kwa kuwa hapo awali walikuwa wakitumia viti mwendo pamoja na vitanda vya matairi ambavyo mara nyingi vilipelekea kutumia muda mrefu kumtoa mgonjwa eneo moja kwenda eneo lingine.