Na Sophia Kingimali
Bodi ya Utalii Tanzania TTB imeishukuru serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha kuibuka mshindi wa bodi bora ya utalii Afrika katika mashindano ya World Travel Award 2023.
Akizungumzia ushindi huo Leo Oktoba 17, 2023 jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Masoko TTB Dkt. Gladstone Mlay amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri kimataifa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa serikali katika sekta ya utalii.
Amesema nchi imeshinda katika vipengele mbalimbali ikiwemo hifadhi bora za taifa ambapo mbuga ya wanyama ya Serengeti imeibuka na ushindi huo.
“Tanzania tumekua tukifanya vizuri sana kimataifa slSerengeti imeshinda nafasi ya kwanza kwa mara ya tano mfurulizo tangu 2019 mpaka sasa huku Ngongoro ikichukua nafasi ya kwanza kivutio bora Afrika”amesema Mlay.
Aidha Mlay ameongeza kuwa pamoja na nchi kuendelea kushinda katika vipengele hivyo vya utaliii imeweza pia kushinda kwa Mara 7 mfurulizo katika kipengere cha visiwa vyenye hadhi ambapo kisiwa cha Thunder kilichopo Mafia ndio kimechukua namba moja Afrika.
Sambamba na hayo Mlay ameongeza kuwa kipengele cha kampuni bora za utalii Tanzania imeshinda ambapo kampuni ya ZARA TOURS ndio imeibuka mshindi.
Naye,Afisa Masoko kutoka ZARA TOURS Nancy Ngotea ameishukuru serikali kwa kuweka juhudi kubwa kwenye sekta ya utalii kwani ndio imeleta ushindi huo kwa taifa.
Aidha Ngotea amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa kutembelea vivutio vilivyopo nchini.
Amesema mafanikio makubwa ambayo yanaendelea kupatikana katika sekta ya utalii yamechochewa na filamu ya the Royal Tour iliyofanywa na Rais Dkt. Samia ambayo imeweza kuifungua nchi kimataifa.