Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akiagalia ramani na baadhi ya wataalamu wa sekta ya ardhi katika Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Singida tarehe 16 Oktoba 2023
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akimsikiliza mmoja wa wananchi wenye mgogoro na Kanisa la KKKT katika eneo la Kipitimo Singida mapema tarehe 16 Oktoba 2023
Sehemu ya washiriki wa utatuzi wa mgogoro baina ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Singida kupitia Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) na mnunuzi wa eneo lenye mgogoro tarehe 16 Oktoba 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (kushoto) akingalia ramani wakati wa kushughulikia migogoro ya ardhi katika mkoa wa Singida tarehe 16 Oktoba 2023. Wa pili kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Singida Shamim Hoza.
Sehemu ya wananchi walioshiriki ziara ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mkoa wa Singida (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
……..
Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Jerry Silaa amesema mkoa wa Singida umetekekeza kwa asilimia 100 Maamuzi ya Baraza la Mawaziri Kuhusu Mgogoro wa Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 975.
Silaa ametoa kauli hiyo tarehe 16 Oktoba 2023 katika viwanja vya Bombadia mkoani Singida mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wa Singida wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya mkoa wa Singida.
Alisema alipoteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Ardhi pamoja na maelekezo mengi lakini moja ni kufuatilia utekelezaji wa Maagizo ya vijiji 975 na Singida ina vijiji 4 ambapo utekelezaji wake umefanyika kwa asilimia mia moja.
‘’Mhe Rais uliponiteua tarehe 30 mwezi wa nane na kuapishwa tarehe 1 Septemba 2023 pamoja na maelekezo mengi lakini ulinipa maelekezo mahsusi moja kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Vijiji 975, nikuthibitishie nilikuja hapa Singida hapa tarehe 6 ya mwezi wa kumi na hapa kuna vijiji 4 na uongozi wa mkoa chini ya Peter Serukamba umetekeleza maagizo hayo kwa asilimia 100’’ alisema Silaa.
Mgogoro wa matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kwa mkoa wa Singida unahusisha Shamba la Kitaraka na wananchi, mgogoro wa vitongoji 3 kuingia Pori la Akiba kwenye msitu wa Swagaswaga, mgogoro wa Bonde la Wembele- Iramba ambapo wananchi wamevamia ardhi oevu kwa ajili ya malisho pamoja na mgogoro wa fidia eneo la chanzo cha maji cha Mwankoko katika manispaa ya Singida.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri Silaa alileza kuwa,amemaliza migogoro miwili mapema kabla ya Maadhimisho ya miaka 60 ya mkoa wa Singida ambapo mgogoro wa kwanza ulihusisha eneo la Manga la Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) lililouzwa kwa Philipo Masawe kwa muhtasari wa kughushi ambapo aliagiza kufutwa kwa hati na kupatiwa JUWAKITA.
Vile vile, Mhe Silaa alielezea mgogoro wa eneo la Kipitimo baina ya wananchi na Kanisa Katoliki la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuweka wazi kuwa, eneo hilo linamilikiwa kwa hati na KKKT tangu mwaka 1955 na kuelekeza pande zenye mgogoro kusimamia sheria na kuheshimu maamuzi.