NA Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amelielekeza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitasaidia kuongeza Pato la Taifa kupitia Sekta ya Michezo.
Mhe. Ndumbaro amesema hayo wakati wa kikao na Baraza hilo kilichofanyika Oktoba 16, 2023 jijini Dar es salaam ambapo ameliagiza lisaidie Vyama na Mashirikisho ya Michezo kupata ushirikiano na Vyama wenza nje ya nchi hatua itakayoviwezesha vyama hivyo kubadilishana uzoefu katika Utawala na uendeshaji wa shughuli za Vyama hivyo.
“BMT pitieni muundo wa uendeshaji michezo kuanzia ngazi ya Mikoa hadi vijiji, michezo iwe ni biashara na ajira, ifike wakati Vilabu vijue idadi ya wanachama wao kwa kuzingatia jinsia ili iwasaidie kujua idadi ya waliyonayo na namna ya kuongeza wanachama wapya” amesema Mhe. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro ametumia nafasi hiyo kuviasa Vyama na Mashirikisho viepuke migogoro ya mara kwa mara badala yake vizingatie Katiba zinazoongoza na kuzingatia Utawala Bora.
Awali, Katibu Mtendaji wa Barza hilo Bi. Neema Msitha amesema Baraza limeendelea kupata mafanikio mbalimbali kwa Timu za Taifa kupitia ufadhili wa Serikali chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kufika mashindano ya Fainali ya Kombe la Dunia kwa Timu ya Wanawake chini ya Miaka 17 pamoja na Timu ya Walemavu.
Bi. Neema ameongeza kuwa kwa sasa Baraza hilo linatumia mfumo wa Kidigitali kusajili Vyama na Mashirikisho ambao umerahisisha gharama na muda wa kufanya Usajili.