Na Muhidin Amri, Kyela
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Mbeya ,umeanza kutekeleza mradi wa maji wa Ngana Group utakaowanufaisha zaidi ya watu 62,000 wa vijiji 25 katika wilaya ya Kyela.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kyela Mhandisi Venance Nkolabigawa alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Oktoba 2022 unatakamilika Disemba 2023 kwa gharama ya Sh.bilioni 7.99 zilizotolewa na serikali kupitia wizara ya maji.
Alisema,mradi huo utakapokamilika utasaidia kutatua kero ya upungufu mkubwa wa maji katika wilaya ya Kyela hasa katika vijiji hivyo ambavyo wakazi wake wana uhitaji makubwa ya maji safi na salama kwa muda mrefu.
Aidha alisema,kukamilika kwa mradi wa maji Ngana kutawezesha kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 70.24 ya sasa hadi kufikia asilimia 85.
Amewatoa hofu wananchi wa wilaya ya Kyela kwa kueleza kuwa,mradi huo siyo longolongo kwani serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iko kazini na imejipanga kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake msimamizi wa miradi ya maji katika wilaya Kyela Mhandisi Felix Msangi alisema, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ruwasa inatekeleza jumla ya miradi saba yenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 8.
Alitaja miradi hiyo inayotekelezwa ni Ngana,Ikombe,Lema,Matema,Kisih
Alisema,upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo ni asilimia 72.4 wakati malengo ya Serikali kufikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 maeneo ya mjini ifikapo mwaka 2025,kwa hiyo kukamilika kwa miradi hiyo kutafikisha malengo yaliyowekwa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kasumulu Nelson Minga,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kutoa fedha kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo ambao utapunguza kero kubwa ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho.
Alisema,kijiji cha Kasumulu kilipata mradi wa maji uliojengwa na wafadhili wa Danida mwaka 1983 wakati huo watu walikuwa 3,000,lakini sasa wameongezeka hadi kufikia 8,500.
Mkazi wa kijiji cha Kasumulu Mawazo Kalinga,ameiomba Ruwasa kukamilisha mradi huo haraka ili wapate huduma ya maji kwenye makazi yao, kwani changamoto ya maji katika kijiji hicho ni kubwa na kuwataka wananchi wenzake kumpa ushirikiano mkandarasi anayetekeleza mradi huo.