Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameagiza ,wakuu wa wilaya, watendaji,maofisa elimu ya watu wazima kuhakikisha wanatilia mkazo na kusimamia mpango wa utoaji wa elimu kwa watu wazima .
Aidha amesema , Wakuu wa Wilaya ni Wenyeviti katika Wilaya hivyo wahakikishe elimu ya watu wazima inatolewa ikiwa hai .
Mkenda aliyasema hayo wakati wa kufunga Kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya juma la elimu ya watu wazima kitaifa lililofanyika Wilayani Kibaha.
Alisema kuwa serikali itaendelea kujenga uwezo na watendaji kwenye Halmashauri kwenye mikoa zitoe kipaumbele kwa program zote za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
“Hakikisheni vituo vile vinavyojihusisha na uzalishaji mali vitambuliwe na kusajiliwa pia kuwe na vifaa,”alisema Mkenda.
Aidha alisema kuwa viongozi wavipe kipaumbele na uhai na viendelee viwe endelevu ili jamii ivitumie kukabiliana na maadui watatu maradhi ujinga na umaskini.
“Watu wakielimika watajiletea maendeleo hivyo vituo hivyo vya elimu ya watu wazima vitumike kwa wananchi kukabili changamoto na kupata ujuzi wa masuala mbalimbali na teknolojia,”alisema Mkenda.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Charles Msonde alisema kuwa moja ya mkazo uliowekwa ni kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanajua kusoma kuandika na kuhesabu.
Msonde alisema kuwa mkazo mwingine ni kuanza kufundisha kufundishwa kiingereza kwa umahiri ambapo matokeo ya darasa la saba ufaulu kiingereza uko chini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Caroline Nombo alisema kuwa jumla ya wanafunzi milioni 5.7 walidahiliwa kwenye elimu changamani kwenye vituo 405.
Nombo alisema kuwa katika kuhakikisha elimu kwa waliokosa zimeanzishwa klabu ambapo wanajifunza KKK na ufundi stadi, ujasiriamali na uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo ambapo hujifunza kuanzia kati ya miezi mitatu hadi mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya program ni pamoja na walimu wa kujitolea kutokuwa na mafunzo ufinyu wa bajeti, upungufu wa vitendea kazi na kushindwa kulipa wa wezeshaji.
Kunenge alisema kuwa mikakati ni kuongeza madarasa kwa kila Halmashauri wanafunzi waliofikia umri wa kwenda shule waandikishwe na jamii inawapokea watoto waliopata changamoto zikiwiwa ni pamoja na mimba, maradhi na nyinginezo.