Mtaalamu Muelekezi wa Sera, Profesa Lindah Mhando, akizungumzia masuala ya sera katika kikao cha tathmini na mapitio ya sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia (2000) na mkakati wa utekelezaji wake (2005), mkoani Singida leo.
Washiriki wa kikao hicho kutoka Wilaya za Iramba, Ikungi na Manyoni wakiwa katika vikundi vya majadiliano
Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Rennie Gondwe (kushoto), akijadiliana jambo na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwajina Lipinga, katika kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho kutoka Wilaya za Iramba, Ikungi na Manyoni wakiwa katika vikundi vya majadiliano
Na waandishi Wetu, Singida
MAMIA ya wadau wameendelea kujitokeza kutoa maoni kuhusu tathmini na mapitio ya sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia (2000) na mkakati wa utekelezaji wake (2005), huku wengi miongoni mwao wakiridhika na mafanikio yaliyofikiwa kwenye eneo la afya ya uzazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakichangia maoni kuhusu tathmini hiyo mkoani hapa leo wadau hao wameomba suala la afya ya uzazi lipewe msukumo na kuwa ajenda ya kudumu na shirikishi kwa kila sekta nchini.
” Sisi kwenye Kata yetu kwa sasa wanawake wengi wanajifungulia kwenye kituo cha afya, na wajawazito wanapatiwa huduma stahiki za maendeleo ya mtoto akiwa tumboni” alisema Samuel Mathayo mkazi wa Kata ya Irisya wilayani Ikungi.
Mkazi mwingine wa Iramba mkoani hapa Ramadhan Abdallah alisema pamoja na juhudi kubwa zilizopo, lakini bado kuna maeneo mengi nchini hususani vijijini yanahitaji maboresho kwenye eneo la afya ya uzazi hasa katika eneo la miundombinu ya barabara na elimu ya jinsia ili kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi.
“Baadhi ya wajawazito waliokaribu kujifungua wanaposafiri kupitia barabara korofi kuelekea zahanati hapo katikati hupoteza maisha” alisema Abdallah.
Aliongeza kuwa elimu kuhusiana na afya ya uzazi na jinsia inapaswa kupewa kipaumbele zaidi kwa wanaume ambao bado muamko wao sio wa kuridhisha.
Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine, ajenda nyingine iliyotawala ni suala la ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusiana na masuala yote yaliyomo ndani ya sera iliyopo, utekelezaji wake hafifu, madawati ya kijinsia kupatikana maeneo ya mjini pekee, mawazo na fikra za mwanamke kuhusu ukatili wa kijinsia bado hazisikilizwi vizuri.
Awali akitoa muongozo wa mchakato huo, Mtaalamu Muelekezi, Profesa Lindah Mhando alisisitiza lengo la tathmini iliyopo ni kuangalia mazuri yaliyofanyika na changamoto zilizopo, na namna ya kuzikabili.
Timu ya wataalamu mbalinbali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto ipo mkoani hapa kwa siku tano mfufulizo ikikutanisha wadau wa makundi yote, ndani ya mikoa ya Kanda ya Kati, mijini na vijijini