Home Mchanganyiko Kikao cha kujadili Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar

Kikao cha kujadili Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame akifungua kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi .

Mkuu wa Kitengo, Mipango Utawala na Rasilimali Watu Haji Faki Hamdani akiuliza suala kwa Afisa wa Mamlaka ya Maji (ZAWA)  katika  kikao  cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi .

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar  kutoka  katika Taasisi mbali mbali wakisikiliza maelezo mafupi ya utekelezaji kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na  Maafa Makame Khatib Makame ( hayupo pichani) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Maruhubi .

…………………

Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatib Makame amezitaka Taasisi mbali mbali zilizojumuishwa  katika mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kufikia azma ya Serikali  ya kuondoa kipindupindu  Zanzibar .

Alisema mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika sekta mbali mbali za Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaimarishwa kwa kudhibiti mazingira hatarishi na kutoa elimu kwa jamii ikiwemo watoto wa skuli .

Hayo aliyasema huko katika ukumbi wa kamisheni ya kukabiliana na maafa maruhubi wakati akifungua kikao cha utekelezaji wa mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar .

Alisema kila taasisi ifanye kazi kwa mujibu wa  mujibu wa mpango huo ili iweze  kurekebisha hali halisi ya mazingira ya mji na vijiji pamoja  na kuweka  mipango mikakati ya utekelezaji wa majukumu hayo.

Aidha alizitaka Taasisi husika ambazo zimo katika mpango wa kutokomeza kipindupindu kutoa elimu endelevu kupitia vyombo mbali mbali vya habari ili jamii iweze kujilinda na uchafu wa mazingira ambao hupelekea kupata maradhi ya mripuko.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alizitaja  hatua ambazo kamisheni itazichukuwa kwa  kufanya ziara katika maeneo mbali mbali ya  Mikoa yote ya Zanzibar ili kuona hali halisi ya utekelezaji wa mpango  kwa Taasisi husika.

Nae muakilishi wa shirika la kuhudumia watoto ulimwenguni (UNICEF)Zanzibar Marko Msambezi alisema ataendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar katika kutekeleza mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar .

Alieleza kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa lengo la kuisaidia jamii pamoja na kuimarisha mazingira ili kuweza kuleta ufanisi

Muakilishi huyo alisema tayari ameshakamilisha ujenga wa vyoo katika maskuli mbali mbali  ya msingi na kuhakikisha vyoo vilivyopo vinakwenda sambamba na idadi ya wanafunzi pamoja na kuahidi kuweka mifereji katika skuli zote ili kuwawezesha wanafunzi kusafisha mikono yao mara kwa mara  .

Pia aliwataka wajumbe hao kuweza kuwasilisha taarifa zao  za utekelezaji wa majukumu kwa kila taasisi husika kwa kila robo kota  ili kuweza kujua utekelezaji mzima wa uratibu wa kipindupindu.

Nao  Wajumbe  wa Mpango huo walisema wanaendeleza na utekelezaji wa mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar  (ZACCEP) Kwa mashirikiano baina ya wizara tofauti  ikiwemo afya mazingira  manispaa, elimu, maji, halmashauri mbali mbali ili kuhakikisha usalama  wa wananchi unapatikana  kwa kuweza kukagua vianzio vya maji na kuweza kuyatibu maji na kutoa elimu ya utumiaji wa dawa za kutibu maji kwa wananchi.

Hata hivyo walieleza kuwa kuna baadhi ya maeneo ya mjini na vijijini  kumebainika kukosekana kwa mashimo ya  maji machafu  jambo ambalo linachangia uchafuzi wa mazingira .

Walisema kuwa  kumezuka utitiri wa uchimbaji holela wa visima katika maeneo  mbali mbali ya mijini,  visima  ambavyo havina uhakika wa  usalama wa maji licha ya  kutolewa elimu ya utumiaji wa dawa kwa wananchi.

Kwa upande wa wajumbe kutoka Pemba walilalamikia changamoto ya ukosefu wa maji  katika Mkoa wa Kusini Pemba walisema  visima vingi vimekauka maji jambo ambalo  huchangia uchafu wa mazingira katika   baadhi ya  vituo vya afya.

Wajumbe wa utekelezaji wa mpango huo walisema wameweza kupiga hatua ya utekelezaji kwa kuunda kikosi kazi cha ukaguzi wa mazingira na kusafisha mitaro na kuzoaji taka katika maeneo mbali mbali ukaguzi wa wafanyabiashara pamoja na sehemu ya biashara zao mabekari ya mikate na kadhalika ili kuhakikisha mpango unatekelezwa .