Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju akikata utepe kuzindua Mitaala mipya kwa miaka mitano kwaajili ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na Wahadhiri kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum jijini Dodoma Oktoba 13, 2023.
Pix 6 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika uandaaji wa Mtaala wa miaka mitano kwa Vyuo vya Maendeleo Mratibu wa zoezi Hilo Abel Palapala wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na Wahadhiri kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum jijini Dodoma Oktoba 13, 2023.
………
Na WMJJWM Dodoma
Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini yake ili waweze kuzalisha wataalamu wenye weledi na sifa stahiki katika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na Wahadhiri kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum jijini Dodoma Oktoba 13, 2023.
Amevitaka Vyuo vyote vinavyotoa taaluma ya Maendeleo ya Jamii kutumia Mtaala huo uliopitishwa na NACTVET ili kuwe na uelewa wa pamoja na kutoa wataalamu wenye sifa zinazotokana na miongozo na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa Mitaala hiyo.
Ameongeza kuwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii mbali na kutoa taaluma ya Maendeleo ya Jamii ila lazima kuwe na uwepo wa somo muhimu la uzalendo na maadili kwa wanafunzi na watumishi katika Vyuo husika ili kujenga Jamii yenye maadili mazuri.
Naye Mwakilishi wa NACTVET Dkt. Edward Mneda ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kufanikisha mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na wahadhiri kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Serikali ili kuzalisha wataalamu hasa wa Kada ya Maendeleo ya Jamii wenye weledi na sifa stahiki.
“Kuwa na Mtaala ni kitu kimoja utekelezaji ni kitu kingine hivyo niwaombe tukatekeleze maboresho ya mitaala kwa ajili ya Vyuo vyetu vya Maendeleo ya Jamii vinavyosimamiwa na Wizara ili tuweze kuandaa wataalamu wanaoendana na soko la ajira na kutatua changamoto za wakati tuliopo” amesema Dkt. Mneda
Akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Neema Ndoboka amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha Wakuu wa Vyuo na wahadhiri kuwa na uelewa wa pamoja wa maboresho ya Mitaala kwa mujibu wa Sheria kwa kila baada ya miaka mitano ili kuendana na wakati na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Ameongeza kuwa katika mafunzo hayo wakufunzi wameelimishwa namna ya kufundishia, kutunga mitihani na kupima uelewa kwa wanafunzi kwa viwango vinavyofanana katika Vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii chini ya Wizara.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na NACTVET na wataalamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa wameendesha mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na wahadhiri kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kuwapa nyenzo muhimu katika kufundisha na kupima uelewa kwa wanafunzi ili kuzalisha wataalamu wenye sifa stahiki.