Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi (hawapo pichani)katika hafla ya utiaji Saini mikataba mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha meli na meli mbili za mizigo, hafla iliyofanyika katika bandari ya Kigoma Mkoani Kigoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la huduma za Meli Tanzania (MSCL) Erick Hamisi (Kulia) na Mkurugenzi wa kampuni ya Dearsan Shipyard Murat Gordt (Kushoto) wakionyesha mikataba iliyosainiwa katika hafla iliyofanyika bandari ya Kigoma Mkoani Kigoma, ambapo miradi mitatu ilisainiwa ambayo ni mradi wa ujenzi wa kiwanda cha meli na ujenzi wa meli mbili za mizigo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la huduma za Meli Tanzania (MSCL) Erick Hamisi (Kulia) na Mkurugenzi wa kampuni ya Dearsan Shipyard Murat Gordt (Kushoto) wakipeana mikono mara baada ya kukamilika kwa shughuli ya utiaji Saini mikataba mitastu ya ujenzi wa kiwanda cha meli na ujenzi wa meli mbili za mizigo katika ziwa Tanganyika na viktoria hafla iliyofanyika katika bandari ya Kigoma Mkoani Kigoma.
….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kusaini mkataba na kampuni ya Dearsan Shipyard ya Uturuki inayotarajiwa kutekeleza miradi mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha kujenga meli na miradi miwili ya ujenzi wa meli za mizigo katika ziwa Viktoria na Ziwa Tanganyika miradi itakayogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 626.
Utiaji saini huo uliofanyika leo umeshuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla iliyofanyika katika Bandari ya Kigoma Ujiji ambapo viongozi mbalimbali wamehudhuria ikiwa ni pamoja na viongozi wa wizara ya uchukuzi, Wabunge wa mikoa ya Rukwa na Kigoma pamoja viongozi wa taasisi mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni wa pekee kwa ukanda wa afrika mashariki na kati na hakuna nchi yenye kiwanda kama hicho, licha ya kuwa meli zetu zikiharibika huwa zinapelekwa Mombasa hata hivyo kiwanda hicho ni kidogo kuliko hiki kinachotarajiwa kujengwa mkoani Kigoma.
“Ujenzi wa kiwanda hiki utasaidia ujenzi wa meli kutoka nchi mbalimbali zinazotuzunguka kama vile Burundi,Zambia, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na nchi zingine mbalimbali kwani kiwanda kitakachojengwa ni kikubwa,” Amesema Waziri Mbarawa.
Aidha Waziri Mbarawa ameitaka MSCL kwenda nchi za jirani kutafuta soko mara kiwanda kitakapokamilika kwani nchi nyingi zinahitaji ujenzi wa meli vinginevyo kiwanda hicho hakitaweza kuwa na ufanisi uliokusudiwa.
Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kurahisisha shughuli za kibiashara kwa nchi ya Tanzania na nchi jirani ambapo mizigo iliyokuwa ikisafiri kwa siku 5 hadi 7 kutoka jijini Dar es salaam hadi nchini Kongo, baada ya mradi kukamilika itaweza kusafiri kwa saa 24 pekee jambo litakalochochea kukua kwa shughuli za kiuchumi.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo akianza na mradi wa ujenzi wa kiwanda cha meli, Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Meli Tanzania (MSCL) Erick Hamis amesema ujenzi huo wa kiwanda unatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 322.7 ambapo amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa na miundombinu ya kudumu ikiwemo chelezo chenye uwezo wa kupandisha na kushusha meli yenye uzito wa tani 5000.
“Kiwanda hiki kitakuwa ni cha kwanza cha aina yake katika ukanda mzima wa maziwa makuu,kiwanda kinatarajiwa kuwa na teknlojia ya kisasa katika ujenzi wa meli ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya kukatia vyuma,” Amesema Hamisi.
Mradi mwingine ni ujenzi wa meli ya mizigo katika Ziwa Tanganyika, ambapo mradi huo umeelezwa kuwa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 158.2 ambapo meli itakayojengwa itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa mpaka tani 3500 huku ikiwa na uwezo wa kubeba malori marefu 25 mradi unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36.
Mradi wa tatu ni ujenzi wa meli nyingine ya mizigo katika Ziwa Viktoria mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 24, unatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 145, ambapo meli hiyo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 3000 za mizigo pia ikiwa na uwezo wa kupakia malori na mabehewa.