Na Mwandishi wetu, Babati
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu, Sera na Bunge, Jenesta Mhagama ameagiza vijana wasiachwe peke yao bali wasaidiwe kupata ubunifu na ujuzi ili kuondoa tatizo la ajira kwa vijana.
Mhagama alitoa agizo hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye maadhimisho ya wiki ya vijana yaliyoanza uwanja wa stendi ya zamani Babati Mkoani Manyara.
Amesema vijana wana uwezo mkubwa kufanya mambo mbalimbali hivyo ili kulinda ubunifu ni kuhakikisha vijana wanapata mitaji ili waendeleze ubunifu wao.
“Tungependa vijana mfanye ubunifu mpya na mataifa yaliyoendelea yalianza na viwanda vidogo vidogo na sisi tuwawekee mazingira mazuri waweze kufanya ubunifu,” amesema Mhagama.
Amezitaka Benki kutoa mikopo nafuu yenye riba nafuu kwa vijana mpaka vijijini ili waweze kufanya mambo makubwa.
Amesema ni vizuri mfuko wa vijana usaidie kuwaibua vijana kwa kuwa ndiyo nguvu kazi ambao wako mil. 21.3 nchi nzima huku akisema asilimia 55.6 ndiyo nguvu kazi ya vijana wa Tanzania.
Ametumia fursa hiyo kuziagiza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya vijana kuwekeza na kuhakikisha miundombinu ya maji, umeme na barabara ni rafiki kwao na yanafikika kiurahisi.
Pia Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu ajira, kazi vijana na watu wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema maadhimisho ya wiki ya vijana yalianza mwaka 2000 ili kuendeleza uzalendo wa waasisi wa nchi.
Prof. Ndalichako amesema wataendelea kuwawezesha vijana mikopo inayotolewa na Olfisi ya Waziri Mkuu.