Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika mdahalo ulioshirikisha Mawaziri wa Jinsia kutoka nchi za wanachama wa umoja wa Afrika wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa kutokomeza Ukeketaji Oktoba 10, 2023 jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mijadala mbalimbali wkatika mdahalo ulioshirikisha Mawaziri wa Jinsia kutoka nchi za wanachama wa umoja wa Afrika wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa kutokomeza Ukeketaji Oktoba 10, 2023 jijini Dar es Salaam.
………
Na WMJJWM, Dar Es Salaam
Tanzania imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike 245 kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya kwa mkoa wa Mara katika msimu wa ukeketaji mwaka jana.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa mdahalo kuhusu jitihada zinazofanywa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji unaovuka mipaka ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa masuala ya Ukeketaji unaoendelea katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam Oktoba 10, 2023.
Katika mjadala huo ambapo washiriki wamepeana uzoefu wa jinsi ya kudhibiti watoto wasiende kukeketwa nje ya mipaka wakati wa misimu ya ukeketaji, Waziri Dkt. Gwajima amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi liliwakamata watu zaidi ya 20 waliohusika na vitendo hivyo na baada ya zoezi hilo, Tanzania imeendelea kutoa elimu kwenye jamii kupitia vyombo mbalimbali vya Habari.
“Lakini haitoshi kusubiri msimu wa ukeketeji watoto wanakimbia wanavushwa mipaka ni lazima tujikite ndani kwenye jamii zetu ambapo Tanzania tumeshatengeneza Mkakati wa Kutokomeza Ukeketaji pamoja na Mpango kazi wake wa utekelezaji wa mwaka 2021 -2025” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Ameeleza kwamba mkakati huo utahusisha elimu na huduma kwa manusura wa ukeketaji pamoja na kufikia hadi ngazi ya vijiji kwa sababu ni suala la ukeketaji limekuwa sio tu mila na desturi bali kwenye imani, uchumi na siasa.
“Jamii haiangalii tena madhara yanayotokana na ukeketaji kwa watoto wetu, suala hili limekuwa kama imani na kutumiwa na baadhi ya wanasiasa pia hivyo elimu kwa viongozi pia muhimu” ameongeza Waziri Gwajima.
Wengine walioshiriki mdahalo huo ni Waziri wa Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii, kutoka Uganda, Mituuzo Peace Regis, Afisa Mtendaji Mkuu wa Masuala ya ukeketaji kutoka Kenya Bernadetha Loloju na Mkurugenzi wa masuala la Wanawake kutoka Ethiopia Seleshi Tadesse.