Na. Lilian Lundo & Issa Sabuni – Mbinga, Songea
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka vijana wa wilaya ya Mbinga kuchangamkia fursa ya mikopo nafuu ya ujenzi wa Vituo vya Mafuta Vijijini inayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mhe. Kapinga amesema hayo leo Oktoba 9, 2023 wakati wa semina ya nishati safi ya kupikia iliyotolewa na Wataalam wa REA kwa Baraza la Umoja wa Vijana na Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.
“Niliona tuje hapa tuongee na kuunga mkono Ajenda ya Mhe. Rais ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala. Nimekuja na Wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wao watatueleza umuhimu wa nishati mbadala, lakini pia watatueleza fursa ambazo zinapatikana, ambazo vijana na wazazi mnaweza kuzitumia,” amesema Mhe. Kapinga.
Amewataka vijana na wazazi walioshiriki semina hiyo kuchangamkia fursa ya mikopo nafuu inayotolewa na REA kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini, ambapo amewataka vijana hao na wazazi kuomba mikopo hiyo ili waweze kujenga Vituo vya Mafuta ambavyo pia vitawaangizia kipato.
Akieleza kuhusu fursa ya mikopo nafuu ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini; Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA, amesema fursa hiyo ni ya mwananchi yeyote anayeishi vijijini. Amesema mikopo hiyo imekuja kutokana na hali ya upatikanaji wa mafuta vijijini kutokuwa salama.
“Vigezo vya maombi ya mkopo huu ni vichache sana. Riba inayotolewa na Serikali ni ndogo, ambayo ni chini asilimia 5 na muda wa kurejesha mkopo ni miaka saba, wakati dhamana ya mkopo ni eneo husika ambalo mradi umejengwa,” amesema Mhandisi Tarimo.
Amesema fedha zinazotolewa kwenye mkopo huo ni shilingi milioni 75 ambazo zinatolewa kwa awamu tatu, ambazo ni awamu ya kwanza na ya pili kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa kituo, na awamu ya tatu ni kwa ajili ya kuagiza mafuta na kuanza biashara, ambapo marejesho yake yanaenda mpaka miaka saba.