Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya, amewataka waamini wa kanisa la EAGT Sayuni kwa Mchungaji Ambangile Kamendu kuacha kutoa rushwa kwa taasisi za serikali na zisizo za kiserikali ili kutokomeza rushwa katika nchi yetu.
Kamanda Mallya ameyasema hayo Oktoba 08, 2023 wakati akitoa elimu ya Ushirikishwaji wa Jamii katika Kanisa hilo ilililopo Vwawa wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.
“Acha kutoa rushwa kwa askari huduma za polisi ni bure, akaongeza kwa kusema usipotoa rushwa hakuna mtu wa kupokea rushwa na ukiombwa rushwa toa taarifa ili nizifanyie kazi kwani rushwa ni adui wa haki” Alisema Kamanda Mallya.
Sanjali na hayo Kamanda Mallya aliwasihi wazazi na walezi walioudhulia ibada kanisani hapo kusimamia malezi ya watoto wao ikiwa ni pamoja na kukaa nao kwa ukaribu ili waweze kuwaambia vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wakiwa nyumbani au mashuleni kama vipigo,kulawitiwa, ushoga na kubakwa kwani kufanya hivyo kutapunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji katika mkoa wetu.
Kwa upande wa waamini wa kanisa hilo wameshukuru sana kwa elimu iliyotolewa na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa jeshi la polisi. Kutoka Dawati la Habari Mkoa wa Songwe.