Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya, amewataka wafanyabiashara na wakulima wakubwa mkoani humo kuweka kamera za ulinzi kwenye maeneo yao badala ya kuajili walinzi wasiokuwa na ujuzi na weledi wa mafunzo na ambao wamezeeka.
Kamanda Mallya amesema hayo Oktoba 7, 2023 wakati wa hafla ya ugawaji vyeti iliyofanyika Tunduma wilayani Momba kwa baadhi ya wamiliki wa silaha za kiraia ambao wanamiliki silaha hizo kihalali.
Hata hivyo kamanda Mallya ameendelea kusisitiza kuwa, katika suala la ulinzi wa mali mbali na kufunga kamera maalum pia ni vyema kuangalia walinzi waliopatiwa mafunzo, wenye afya njema, weledi katika kufanya majukumu hayo.
Aidha, kamanda Mallya amewaagiza Wakuu wa Polisi wa Wilaya mkoani humo kuendesha mafunzo maalum ya ulengaji wa shabaha kwa wamilikia hao wa silaha za kiraia yatakayolenga kuwakumbusha matumizi sahihi ya silaha hizo na kutokuzitumia kwa matumizi mengine ambayo ni kinyume na kanuni, sheria na taratibu za umiliki wa silaha za kiraia.
Zoezi la ugawaji wa vyeti hivyo limefanyika baada ya wamiliki hao wa silaha za kiraia kupewa mafunzo ya wiki moja yaliyofunguliwa tarehe 7 Agosti 2023 na kuhitimishwa rasmi Agosti 12, 2023.