Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (katikati)Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM), (kulia) na Mwakilishi wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) Kiomboi Iramba John Leonard wakikata keki maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yaliyoandaliwa na NSSF Oktoba 6, 2023,
…………………………………………………..
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAKATI maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yakiadhimishwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Singida limezitambua taasisi na kuwashukuru waajiri wanaojitolea kwa hali na mali kuhakikisha michango ya wanachama wake inawasilishwa kwa wakati.
Hata hivyo shirika hilo pamoja na mambo mengine limezitaja taasisi
takribani tano zilizoongoza kwa uwasilishaji wa michango hiyo kwa mwaka huu Mkoani hapa zikiwemo Mount Meru Miller na Tree for the Future.
Nyingine ni Makiungu Hospital, Srs
Medical Missionaries of Mary (MMM), na Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) Kiomboi Iramba ambazo zimetunukiwa vyeti vya kutambua mchango huo.
Hata hivyo akizungumza wakati wa utoaji wa vyeti hivyo Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa alianisha sababu za utoaji wa tuzo hizo kuwa taasisi hizo zimekuwa zikitekeleza sheria za NSSF kwa kupeleka michango na kuandikisha wanachama kwa wakati.
“Wapo waajiri wakubwa na wadogo wenye michango mikubwa kabisa na wenye michango midogo lakini hawa wamefanya vizuri zaidi,” alisema Kalimilwa.
Kalimilwa alihimiza waajiri kufuata sheria za NSSF na kuwataka kutekeleza
takwa hilo la kisheria kwa mustakabari wa maslahi bora ya wafanyakazi wao pindi wanapo staafu.
Baadhi ya waajiri waliopata vyeti hivyo, Otomali Haule kutoka Hospitali ya
Makiungu, Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM), waliishukuru NSSF kwa kutambua mchango na kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo baina ya pande zote mbili ambapo walitoa wito kwa taasisi
zingine kujenga tabia ya kupeleka michango yao katika mfuko huo.
Tukio hilo la kuzitunuku vyeti vya heshima taasisi hizo limeambatana na
kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2023 ambayo yamebeba ujumbe usemao ‘Ushirikiano kwa Huduma Bora, ‘Team work for service
Excellency’ .