Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa Hamis Shabani Msabaha (maarufu kama Muna Dalali), ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza na wana CCM wa Mtaa wa Unyika katika mkutano mkuu wa Tawi hilo uliofanyika Oktoba 6, 2023.
…………………………………………..
Na Dotto Mwaibale, Singida
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa Hamis Shabani Msabaha (maarufu kama Muna Dalali) amekabidhi Kiwanja chenye thamani ya Sh.Milioni 3 kwa wanachama wenzake wa CCM wa Tawi la Unyinga Kata ya Mandewa Manispaa ya Singida mkoani hapa.
Msabaha ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya Kata ya Mandewa, mjumbe wa mkutano mkuu Wilaya ya Singida Mjini na Mlezi wa CCM Tawi la Unyinga amefikia hatua hiyo kutokana na mapenzi yake binafsi kwa CCM na maono chanya katika kuhakikisha chama hicho chini ya Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kinaendelea kustawi kwa manufaa ya watanzania.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho Tawi la Unyinga ambapo
alipokea taarifa ya chama aliwataka wana CCM kujenga tabia ya kujitoa na
kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa ipasavyo.
Mbali ya kutoa kiwanja hicho Msabaha alishiriki chakula cha pamoja na kutoa
misaada kwa wazee wasiojiweza na kwa wajumbe wenzake mbalimbali kama ishara ya upendo na ushirikiano lengo likiwa ni kuleta maendeleo katika tawi hilo na Singida
kwa ujumla.
Aidha, Msabaha alitoa saruji mifuko 150 kwa ajili ya kuanza kujenga msingi
wa ofisi hiyo na akawaomba wana CCM wenzake kujitoa ili kukamilisha ofisi hiyo na kuanza kutumika katika muda mfupi ujao.
Baadhi ya watu waliohudhuria shughuli hiyo akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mandewa, Omari Said, walimshukuru Msabaha kwa kuwa na moyo wa kujitoa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii na akaomba watu wengine kuiga tabia hiyo.
Katika mkutano huo Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kata ya Mandewa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Smaujata, Idara ya Uhitaji, Maafa na
Makundi maalumu, Ramadhani Mdanku walipata fursa ya kuelezea ukatili wa
kijinsia na kukithiri kwa vitendo vya watoto wa kiume kulawitiwa na hatua
ambazo zinapaswa kuchukuliwa kwa wazazi na walezi ili kukabiliana na vitendo hivyo.
Aidha, Mkuu wa Polisi Kata ya Mandewa, Mkaguzi wa Polisi Ramadhani Hemba, aliwahimiza wazazi na walezi
kusimamia malezi ya watoto wao na kueleza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa kulawitiwa watoto wa kiume vimezidi kuongezeka na wahusika wakiwa ni ndugu au jamaa wa karibu wa waathirika hao.
Hemba alitoa wito kwa jamii kutoa taarifa mara moja pale watakapoona
vitendo hivyo ili sheria ichukue mkondo wake au wapige simu bure namba 116.
“Serikali imeshusha huduma za Jeshi la Polisi hadi ngazi ya chini
kabisa kwenye kata kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hivyo msiogope kutoa taarifa za kihalifu ili muweze kusaidiwa kwani sisi polisi ndio wenye wajibu wa kushirikiana na ninyi katika kukabiliana na vitendo hivyo,” alisema Hemba.
Katika mkutano huo burudani mbalimbali zilikuwepo zikitolewa na kikundi cha Sanaa cha Makhirikhiri, Smaujata ambao waliimba shairi na kikundi cha ngoma za
asili cha kabila la Wanyaturu cha Misake ambacho kilionesha umahiri mkubwa wa kucheza na kuimba.
Katibu wa UVCCM Kata ya Mandewa, Yusuph Nkii, akizungumza. |