Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala ameiagiza wakala wa barabara za mijini na vijijini TARULA kukarabati na kuweka mpango madhubuti utakaosaidia kupitika muda wote kwa barabara za mitaa ya kata ya Mecco
Ametoa agizo hilo wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo katika kata ya Mecco ambapo amesema kuwa licha ya kata ya hiyo kuwa katikati ya mji bado inakabiliwa na changamoto za barabara za uhakika
‘.. Hali ya barabara sio rafiki sana kwa kata ya Mecco, Kata ipo mjini lakini ina changamoto za barabara sasa ni lazima kero hii tuimalize ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala amewataka wataalam wa Ardhi na mipango miji wa manispaa ya Ilemela kuhakikisha wanazisimamia vizuri kampuni za upimaji shirikishi Ili kuzuia vitendo viovu kwa baadhi ya wananchi vya kusogeza vigingi vya mipaka katika maeneo ya barabara
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARULA wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe amesema kuwa wamekuwa wakiendelea na juhudi za kutengeneza barabara za wilaya hiyo licha ya uwepo wa changamoto ya kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na uhitaji ambapo wamefanikiwa kujenga barabara yenye urefu wa mita 264, mitaro mita 213, karavati moja kwa thamani ya shilingi milioni 43 fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa kata ya Mecco wakati barabara kubwa ya Lami ya Nundu nayo ikikarabatiwa na kmpuni ya JASCO
Godlisten Kisanga ni diwani wa kata ya Mecco ambapo ameishukuru Serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata yake pamoja na kuwaomba wananchi kuiunga mkono
Nae Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Ndugu Charles David amesema kuwa Mbunge wa Jimbo hilo amekuwa akichangia shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya kata hiyo ikiwemo tofali 2500 kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya kata, ametoa tofali za ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Nyamwilekelwa na jengo la ofisi ya mtaa wa Nundu
Mkuu wa wilaya ya Ilemela amefanya ziara katika kata za wilaya hiyo Kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo akiwa ameambatana na wakuu wa idara na vitengo wa manispaa ya Ilemela, wakuu wa taasisi zilizopo ndani ya wilaya hiyo kama Tanesco, MWAUWASA, TARULA na Kamati yake ya ulinzi na usalama