BEBKI ya NMB imeanzisha dirisha maalumu la kuwahudumia Watanzania wanaoishi nje ya nchi, huduma ambayo Serikali imesema itasaidia kuongeza fedha diaspora wanazotuma na kuwekeza nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Suluhisho hilo linaloitwa NMB Kwetu limezinduliwa rasmi mwishoni wiki iliyopita ili kutoa huduma za kifedha kwa diaspora kwa kuwapa nafasi ya kufungua akaunti na kufanya miamala kidijitali pamoja na kuweza kuwekeza nyumbani kupitia benki hiyo.
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Mbundi, aliyemwakilisha Waziri January Makamba.
Kiongozi huyo amesema mbali na huduma hiyo kurahisisha utumaji wa fedha pia itaongeza fedha hizo za kigeni wanazotuma wana diaspora nyumbani.
“NMB Kwetu ni huduma muhimu inayoenda kusaidia juhudi za serikali za kuhakikisha Watanzania wote popote walipo wanapata huduma za kifedha, wakiwemo wale wanaoishi ughaibuni,” alisema Balozi Mbundi
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua na kuthamini mchango wa diaspora katika ujenzi wa taifa kupitia utaalamu wao na fedha wanazotuma nyumbani ambazo zilifikia dola za kimarekani milioni 369.3 mwaka 2021.
Balozi Mbundi alisema kiasi hicho kimekuwa kinaongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia dola bilioni 1.1 sawa na TZS trilioni 2.6 mwaka jana ambapo diaspora walitumia TZS bilioni 4.4 kuwekeza katika ununuzi wa nyumba na viwanja nchini.
Aliongeza Watanzania hao pia ni washiriki wazuri katika soko la mitaji na hisa ambapo mwaka 2022 waliwekeza TZS bilioni 2.3 kwenye Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT).
“Bila shaka diaspora wetu watachangamkia na hatifungani ya NMB Jamii Bond ambayo sasa hivi iko sokoni,” alisema Balozi Mbundi akitambua mchango wa Benki ya NMB katika shughuli za maendeleo.
Alisema mbali na kuwa jambo la kihistoria, huduma ya NMB Kwetu pia imekuja wakati muafaka na inatoa fursa kwa benki hiyo kunufaika na miamala ya kimataifa.
Balozi Mbundi alisema kipengele cha bima ya maisha cha suluhisho hilo kitatua changamoto ya muda mrefu ya wana diaspora pindi walipokuwa wakikabiliwa na madhira ya vifo au ulemavu wa kudumu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema mbali na fao la kifo na ulemavu, bima hiyo pia inagharamia usafirishaji wa maiti huku akitaja sifa kubwa ya kwanza ya NMB Kwetu kuwa ni kutengeneza mfumo wa kidijitali wa ukusanyaji wa nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kufungua akaunti.
“Suluhisho la pili kupitia NMB Kwetu, ni Bima ya Maisha. Wana diaspora wote watakaofungua akaunti zao Benki ya NMB moja kwa moja watakuwa wameingia bima ya maisha yenye thamani ya hadi TZS milioni 29. Bima hii ya maisha inatolewa kwa ushirikiano na Kampuni ya Bima ya Sanlam Life.”
Akaunti zote za NMB Kwetu hazitakuwa na makato ya kila mwezi kama akaunti nyingine, Bi Zaipuna alifafanua na kusema utumaji wa fedha utaongezewa ufanisi na huduma ya Worldwide Pesa.
NMB ilianzisha huduma hii inayowezesha wana diaspora kutuma pesa nyumbani kwa ndugu, jamaa na marafiki kutoka nchi zaidi ya 100 duniani mwaka jana kwa kushirikiana na kampuni za Thunes na Terrapay.
Pamoja na kutotangazwa, Bi Zaipuna amesema mpaka sasa Worldwide Pesa tayari imefanikisha zaidi ya miamala 35,000 yenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 52.
“Fursa za uwekezaji kwa wenzetu waliopo diaspora pia ni kipaumbele chetu. Kupitia NMB Kwetu, wateja wetu, wana Diaspora watapata fursa ya kupata mikopo ya nyumba, fursa za kuwekeza kwenye amana za muda mfupi na na amana za muda mrefu zenye viwango shindani na na nyingi pia zikiwa na Bima ya Maisha,” alisisitiza.