Mganga Mkuu wa Hospitali ya Jamii Kiuma Mzelifa Masaga akizungumza kuhusu maboresho makubwa ya huduma za matibabu yliyofanyika katika Hospitali hiyo ikiwemo huduma ya kuunga mifupa kwa watu wanaopata ajali.
Moja ya vitanda vilivyofungwa kwenye chumba maalum cha upasuaji katika Hospitali ya Jamii Kiuma wilayani Tunduru.
Baadhi ya wataalam wa mionzi wakionyesha vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya uchunguzi.
………
Na Muhidin Amri,
WILAYA ya Tunduru ni moja ya wilaya tano zinazounda mkoa wa Ruvuma na kati ya wilaya kongwe hapa nchini iliyoanzishwa na Serikali ya wakoloni wa Kijerumani mwaka 1905.
Wilaya hii inatajwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini,misitu,ardhi bora,mito inayotiririsha maji majira yote ya mwaka na wanyama wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Hata hivyo,licha ya utajiri huo lakini rasilimali hizo hazijawanufaisha wenyeji wa Tunduru kutokana na ukosefu wa elimu ambayo ingewawezesha kufahamu na kutumia vyema rasilimali ili kujiletea maendeleo ya mmoja mmoja na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Kutokana na hali hiyo Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi,limeona ipo haja ya kuwafungua macho wakazi wa wilaya ya Tunduru kwa kuanzisha huduma za kijamii kama vile Hospitali, shule na chuo cha ufundi.
Lengo la Kanisa kuanzisha huduma hizo ,ni katika kutekeleza adhima yake ya kuimarisha huduma za kimwili kwa kuwapatia ujuzi na maarifa ambayo yatawasaidia kuzitumia rasilimali zao kuondokana na maadui watatu(umaskini,ujinga na maradhi).
Askofu wa Kanisa hilo Noel Mbawala anasema,wakati kanisa linaanzishwa mwaka 1996,walianza kutoa huduma za kiroho baada ya kubaini kuwa katika tarafa ya Matemanga hakuna huduma hiyo hasa kwa Wakristu ambao walilazimika kwenda mbali na makazi yao.
Kwa mujibu wa Askofu Mbawala,jambo hilo ni muhimu kwani wanatambua mtu mwenye imani na hofu ya Mungu ni rahisi kushika na kupokea huduma za kimwili katika kukabiliana na umaskini wa kipato kuanzia ngazi ya familia.
Hata hivyo anaeleza kuwa,kutokana na waumini na jamii inayoishi kuzunguka eneo hilo kuhitaji huduma ya kimwili wakaamua kupanua wigo na kuanzisha huduma za kijamii ikiwemo Hospitali,chuo cha ufundi,chuo cha uuguzi na shule ya sekondari.
Anaeleza kuwa,kwa ujumla huduma hizo zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii siyo ya wana Tunduru tu,bali kwa wananchi wa wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma,wanaosafiri kwa kutumia Barabara kuu ya Songea-Tunduru na wa mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara wanaotumia huduma za kanisa kupitia taasisi ya Kiuma kama suluhisho la matatizo waliyonayo.
Anataja,Hospitali ya jamii Kiuma iliyoanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kutoa huduma za afya kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ambao wanashindwa kwenda maeneo mengine kupata huduma kutokana na umbali uliopo au gharama kubwa za matibabu.
“Hospitali hii imesaidia sana kupunguza vifo vya watoto na mama wajawazito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, wana jamii ya Milonde na wananchi wa tarafa nzima ya Matemanga kwa sababu hata gharama za matibabu ni ndogo ikilinganishwa na gharama zinazotolewa kwenye Hospitali nyingine”anasema.
Askofu Mbawala anasema,Hospitali hiyo imesaidia sana kusogeza huduma za afya kwa wananchi ambao kwa sasa hawapati usumbufu wa kwenda hadi Hospitali ya wilaya Tunduru mjini umbali wa kilomita 64 na kilomita 200 kwenda Hospitali ya Rufaa Songea(Homso) kufuata matibabu.
Anaongeza kuwa,hata mama wajawazito wanapata nafasi ya kuhudhuria kliniki baada tu ya kuhisi ujauzito tofauti na hapo awali ambapo baadhi yao walishindwa kuhudhuria kwa wakati kutokana na umbali uliokuwepo.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Kanisa la taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta anasema,uanzishwaji wa huduma za kijamii unalenga kutimiliza neno la Mungu ambalo siyo kuhubiri tu bali kusaidia huduma za kijamii kwa watu wenye mahitaji ya kimwili na akili ili waweze kumjua Mungu.
Anasema,kanisa liliona kuna umuhimu mkubwa wa kuanzisha huduma za afya ikizingatia eneo la Milonde lilikuwa kama limejitenga,hivyo kuwa vigumu kwa jamii kupata huduma za afya kwa haraka hasa akina mama wajawazito.
“wakati huo wilaya yote ya Tunduru kulikuwa na Hospitali mbili tu ambazo ni Hospitali ya wilaya na Hospitali ya Misheni Mbesa,hivyo kanisa la Upendo kupitia taasisi yake ya Kiuma ikaona ni vema kuanzisha Hospitali ili kusogeza huduma za afya kwa waumini wake na jamii kwa ujumla”anasema.
Anataja umbali kutoka Milonde hadi Tunduru mjini ambako inapatikana Hospitali ya wilaya ni kilomita 61,na kwenda Songea mjini makao makuu ya mkoa ni kilomita 200, hivyo wananchi wengi walipoteza maisha kwa kushindwa kufika Hospitalini kwa wakati.
Anasema,kwa sasa Hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja na lengo ni kutoa huduma za kibingwa badala ya kuishia kutoa huduma za kawaida,kwani mahitaji ya huduma za kibingwa ni kubwa na zinatolewa katika Hospitali ya rufaa Songea na Hospitali ya Ndanda.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Jamii Dkt Mzelifa Masaga anasema,Hospitali ya Jamii Kiuma kwa kutambua mabadailiko ya Dunia ya sasa Hospitali ya Jamii inaendelea kupanua na kuboresha huduma zake ili wananchi wafurahie huduma zinazotolewa.
Kwa mujibu wa Dkt Masaga, katika kukabiliana na ushindani wa huduma Hospitali hiyo ndiyo ya kwanza wilayani Tunduru kutoa huduma za kuweka vyuma kwa wagonjwa waliovunjika mifupa baada ya kupata ajali.
Dkt. Masaga anasema,wamekuwa wakitumia teknolojia kwenye magonjwa ya mifupa ambayo inasaidia mgonjwa kupona haraka na kuendelea na shughuli zake za uzalishaji mali kwa muda mfupi.
“kimsingi Hospitali yetu inaendelea kutoa huduma ambazo ni za kijamii kwa gharama ndogo ambazo kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuzifikia ikilinganisha na gharama zinazotolewa na Hospitali nyingine katika ukanda wetu wa kusini”alisema Dkt Masaga.
Alitaja baadhi ya huduma zinazotolewa ni za kimaabara,huduma za mionzi(X-ray)na Utra Sound,huduma za wagonjwa wa nje(OPD)kulaza wagonjwa ambapo jumla ya vitanda 111 vilisajiliwa na huduma za upasuaji ikiwemo tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa.
Aidha anasema,wanafanya operesheni kwa wanawake wanaoshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida,operesheni za uvimbe na vipimo kwa akina mama wanaoshindwa kushika mimba na huduma zote zenye hadhi ya Hospitali.
Dkt Masaga,anaishukuru Halmashauri ya wilaya Tunduru kuwapatia mtaalam wa meno ambaye amewezesha Hospitali,na wananchi kuanza kupata huduma za meno ambayo haikuwepo tangu Hospitali hiyo ilipoanzishwa.
Katibu wa Hospitali hiyo Mbarouk Maulid Seleman anasema,katika kutekeleza maagizo na mwogonzo wa serikali wameanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliojiunga na Bima ya afya na wametenga wodi maalum kwa ajili yao.
Anasema,hatua hiyo imesaidia sana kuboresha huduma za afya kwa wanachama wakiwemo watumishi wa taasisi ya Kiuma,watumishi wa serikali na wanafunzi ambao ni lazima wawe na Bima ya afya kwa ajili ya matibabu kabla ya kujiunga na shule ya sekondari.
Anasema wodi maalum ya wagonjwa wanaotumia bima, imevutia na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya baada ya kushuhudia huduma nzuri zinazotolewa ikiwemo kupungua kwa gharama za matibabu ,tofauti na wagonjwa wasiokuwa wanachama ambao wanaolazimika kwenda na fedha nyingi mifukoni ili kugharamia matibabu.
Mkazi wa Milonde Anitha Nchimbi anasema,kuanzishwa kwa wodi ya Bima imekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu katika Hospitali hiyo kwa sababu kwenye wodi mchanganyiko siyo rahisi kupata huduma kwa haraka.
Hata hivyo,anauomba uongozi wa Hospitali hiyo kuendelea kufanya maboresha ili iwe msaada mkubwa zaidi kwa jamii ya wana Kiuma na wananchi wa maeneo mengine wanaofika ili kupata matibabu