Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Nelson Mlali akizungumza katika kikao kazi kati ya shirika hilo, Ofisi ya Masajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mafao House Ilala jijini
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri TEF Bw. Deodatus Balile akitaka ufafanuzi wa baadhi ya mambo katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mafao House Ilala jijini Dar es Salaa leo Oktoba 5,2023.
Afisa habari kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akielezea baadhi ya mambo wakati kikao hicho kikiendelea.
Meneja Masoko na Mawasiliano Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bi. Mariam Mwayela akiwashukuru wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri TEF mara baada ya kikao hicho kumalizika.
…………………………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanikiwa kuchangia shilingi bilioni 43 kutoka bilioni 9 katika mfuko mkuu wa serikali pamoja na kutekeleza mradi wa kimataifa ya mawasilino na uchukuzi katika Ziwa Victoria ukiwa na lengo la kuboresha mawasiliano hasa inapoekea ajali na kutoa taarifa kwa wakati ili msaada wa karibu uweze kufika.
Akizungumza leo Oktoba 5, 2023 katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jakwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Jengo la Mfao House Ilala jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Nelson Mlali, amesema mradi huo umelenga kuwasaidia wavuvi na wasafirisha mzigo ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na serikali ya Uganda.
“Tunatekeleza ujenzi wa boti tano za uokozi ambapo ziwa Victoria kutakuwa na boti mbili, Tanganyika boti mbili, Nyansa boti moja ambazo zitakuwa zinakimbia kufanya shughuli za uokoaji” amesema Bw. Mlali.
Bw. Mlali amesema kuwa wamefanikiwa kuunda nyenzo za udhibiti ikiwemo kanuni na sheria mbalimbali lengo ni kuhakikisha usafiri wa maji unakuwa salama.
Bw. Mlali amesema kuwa idadi za leseni za watoa huduma imeongezeka kwa asilimia kubwa na kusababisha mapato ya serikali kuongezeka kutokana na usajili unaofanyika.
Amesema kuwa pia wataalamu wameongezeka kwenda kuongeza nguvu katika kutoa huduma sekta ya usafiri kwa njia ya maji.
“Idadi ya leseni ya vyombo vidogo vya usafiri kwa njia ya maji imeongezeka, watu wengi wanaomba kukata leseni kwani awali walikuwa wanafanya kazi kwa kujificha bila kuwa na kibali” amesema Bw. Mlali.
Amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa meli za kigeni na ndani ya nchi ili kuhakikisha meli hizo zinaondoka zikiwa salama bila kupata hitalafu ya kiufundi.
“Ripoti zetu za ukaguzi wa meli zinaheshimiwa na bandari mbalimbali duniani, hivyo meli zikienda zinapokelewa na kupata ushirikiano kulingana na ripoti ya ukaguzi” amesema Bw. Mlali.
Amesema kuwa wanaendelea kusimamia miongozo, mikataba na itifaki kwa ajili ya kutekeleza mikataba ya kimataifa ambayo imeridhiwa na Taifa.
“Tunazuia umwagikaji wa mafuta baharini ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kuathiri usafiri kwa njia ya maji pamoja na viumbe hai” amesema Bw. Mlali.
Amesema kuwa wamepata hati safi kutoka kwa mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) pamoja na kupata tuzo ya mshindi wa kwanza katika mashirika ya umma katika mahesabu ya fedha inayotolewa na NBAA pamoja cheti bora za mifumo.
Pia wamefanikiwa kuwa miongoni mwa taasisi 10 bora katika mashirika ya umma katika mwaka wa fedha 2020/21 baada ya ukaguzi uliofanya na PPRA.
“Mafanikio hayo yanatokana na ubora wa huduma tunayofanya, TASAC tunafanya kazi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usafiri kwa njia ya maji unakuwa salama” amesema Bw. Mlali.
Amesema kuwa wamefanikiwa kufanya sensa ya usafiri wa vyombo vidogo vya majini ambapo imeonesha asilimia 88 ni vile venye urefu wa mita nne, huku akieleza kuwa wataendelea kutoa taarifa kuhusu vyombo hivyo ili kufanya maboresho ya kuboresha katika sekta ya usafiri wa majini.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yametokana usikivu wa serikali ya Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani katika kupokea ushauri wa serikali wa kitaalamu na kutoa maelekezo sahihi kupitia Wizara ya Uchukuzi.
“Wataalamu wakishauri jambo wanaliangalia na kulitekeleza na matokeo yake tunayaona, pia tunafatilia miongozo inayotolewa na serikali na kamati mbalimbali za bunge wanapotutembelea na kutushauri” amesema amesema Bw. Mlali.