……………….
Na Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Uhifadhi la Taifa nchini (TANAPA) imeendela kujizatiti kikamilifu katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wake na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wanchi.
Akifunga Mafunzo ya Ukarimu kwa watendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa niamba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba ameipongeza TANAPA kwa hatua hiyo nzuri kwa maendeleo ya Utalii.
Kamishna Wakulyamba ameongeza kuwa kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour inachochea ongezeko kubwa la watalii nchini, hivyo amewataka watumishi waliopata mafunzo hayo kuyatumia vyema katika kuwahudumia wageni hao.
“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kutosha katika utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kufikia matarajio yao na mtaenda kushughulikia masuala mbalimbali ya wateja kwa wakati, kudumisha mahusiano ya kibiashara, kuvutia wawekezaji, kuongeza idadi ya watalii na mapato” Alisema Kamishna Wakulyamba
Aidha Kupitia vivutio lukuki vya Utalii nchini Kamishna Wakulyamba amebainisha kuwa, sekta ya utalii imeendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali na uchumi kwa ujumla.
“Kutokana na mchango wa sekta ya Utalii katika pato la Taifa, fedha za kigeni, uwekezaji na ajira, ambapo sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa (GDP), asilimia 25 ya mauzo yote ya nje, asilimia 60 ya mapato yote yatokanayo na biashara za huduma na kuzalisha takriban ajira milioni 1.6 za moja kwa moja na ambazo si za moja kwa moja”. Alibainisha Kamishna Wakulyamba.
Akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA, Herman Batiho ameeleza kuwa mafunzo hayo ya siku 3 na kudhaminiwa na Banki ya Azania yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa TANAPA hasa katika nyanja ya Ukarimu kwenye utoaji huduma kazini.