Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na ubunifu wizara ya elimu sayansi na teknolojia, Prof .Ladslaus Mnyone akizindua kituo hicho jijini Arusha.
Aliyeko katikati ni Mkurugenzi wa sayansi ,teknolojia na ubunifu wizara ya elimu ,sayansi na teknolojia ,Prof .Ladslaus Mnyone akitembelea kituo hicho mara baada ya uzinduzi huo jijini Arusha
………
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha .Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imezindua kituo cha elimu kwa njia ya kidigitali (C-CoDE) ambacho kimegharimu zaidi ya dola laki moja na kitatumika kwa ajili ya walimu kuandaa vipindi ambavyo vitafundishwa kidigitali.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Makamu mkuu wa Taasisi hiyo,Prof Maulilio Kipanyula wakati akizungumza katika uzinduzi huo mkoani Arusha.
Prof .Kipanyula amesema kituo hicho kitatumika kufundisha walimu na wakufunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kufundisha kidigitali.
Ameongeza kituo hicho kimefadhiliwa na serikali ya Uswisi kwa kushirikiana na vyuo viwili kutoka Uswisi na Morocco ambapo kituo hicho kitakuwa msingi na cha kihistoria kwani ni jambo ambalo walikuwa wanatamani kutoa elimu kidigitali kwa muda mrefu.
“Elimu ya kidigitali inawezesha watu kupata maarifa kwa usawa wakiwa popote nchini na kituo hiki kitakuwa ndio mwarobaini wa kuleta chachu kwa taasisi zingine nchini kuanza kutoa elimu kidigitali.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo ,Mkurugenzi wa sayansi Teknolojia na ubunifu wizara ya Elimu ,sayansi na Teknolojia ,Prof .Ladslaus Mnyone amesema kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo kinapaswa kupongezwa na kuigwa na taasisi zingine kwani hivi sasa serikali inasisitiza sana taasisi na vyuo kuwekeza katika kutoa elimu kidigitali ili iweze kumfikia kila mmoja popote pale alipo.
Amesema nafasi ya teknolojia ni ya muhimu sana katika taasisi mbalimbali kwani zinawezesha utoaji wa elimu kwa haraka na kumfikia mhusika kwa njia rahisi akiwa sehemu yoyote na kuweza kupata vijana wenye umahiri wa hali ya juu.
“Kuna wadau wengi wanahitaji kuunga mkono juhudi za serikali tunawakaribisha sana na milango ipo wazi kwa ajili ya kufanya majadiliano na kuangalia namna ya kufanya na kuhakikisha kila kijana wa kitanzania anapata elimu akiwa mahali popote pale.”amesema.
Naibu Makamu mkuu wa chuo -Utafiti (UDSM) Prof .Nelson Boniface amesema kupitia kituo hicho watanzania wengi wataweza kupata elimu kwa njia ya kidigitali kwani ni kituo cha mfano na ni cha kipekee kwa nchi yetu .
“Kuna vituo vitatu tu kwa Afrika Mashariki na hiki ni kituo cha kwanza kwa Tanzania kinachotoa elimu kwa njia ya kidigitali ili kuweza kuwafikia watanzania wengi walioko katika maeneo mbalimbali wakiwemo walioko vijijini pia na sisi tumekuja kujifunza kwa wenzetu ili tuweze kushirikiana nao .”amesema