Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo,Dkt. Margaret Mutaleba Martin akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha.
Wahitimu wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Sokon 11 wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahafali hayo.
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha .Wazazi pamoja na walezi wametakiwa kuacha kuwa bize na shughuli za maendeleo kila wakati na kusahau majukumu ya kuangalia watoto wao jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa malezi mabaya kwa watoto wao.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari sokon 11,Dk Margaret Mutaleba Martin wakati akizungumza katika mahafali ya kidato cha nne ambapo jumla ya wanafunzi 151 walihitimu kidato cha nne.
Amesema kuwa,watoto wengi wamekuwa wakiharibika kutokana na malezi mabovu ndani ya familia nyingi ambayo yanachangiwa na wazazi wenyewe kwa kutopata muda wa kuangalia watoto wao na kuwa bize na shughuli za kijamii kila wakati.
“Mimi sikatai wazazi wasiwe bize kutafuta hela ila sasa sio kuwa bize kiasi kwamba unawasahau na watoto na kuwapa uhuru ambao mwisho wa siku ndio unawaharibu na wanaishia pabaya na kushindwa kufikia malengo yao waliyojiwekea, hivyo naombeni sana muwe makini na watoto na pia mtenge muda wa kuzungumza nao ili nao wawe wawazi katika kuwaelezea changamoto zao wanazokabiliana nazo kwenye jamii.”amesema.
Kaimu mkuu wa shule ya Sokon 11 Geofrey Mvamba ,amesema kuwa, shule hiyo ilianzishwa mwaka 2015 kutokana na mawazo ya viongozi wa kijiji hususani muasisi Obedi Melami wakati huo akiwa Mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye kwa sasa ni Diwani wa kata ya Sokon 11 akishirikiana na wapenda maendeleo.
Amesema shule hiyo ilianza na wanafunzi 53 ambapo sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 881 ambapo wananchi wa kijiji cha sokon 11 waliweza kuanzisha shule hiyo ambapo walifanikiwa kuchangia shs 480,000,000 huku serikali na wadau wakichanga 330,000 ,0000 na wafadhili kutoka ubalozi wa japan wakichanga 196,257,010 ambapo hadi sasa hivi tangu kuanzishwa kwa shule hiyo ujenzi wa shule hiyo umeshagharimu zaidi ya shs 1.6 bilioni.
Amesema kuwa ,kiwango cha ufaulu shuleni hapo kimekuwa kikiongezeka kila mwaka kutokana na ufundishaji mzuri unaofanywa na walimu shuleni hapo huku walimu wakitoa motisha kwa wanafunzi kuhusu kupenda masomo ya sayansi jambo ambalo limechangia kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaopenda masomo ya sayansi.
Mvamba amesema, pamoja na mafanikio mbalimbali bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa viwanja vya michezo, ukosefu wa maktaba,bwalo la chakula,ukosefu wa mabweni, na ukosefu wa nyumba za walimu , huku walimu wa somo la hisabati wakiwa hawatoshi pamoja na kutokuwa na uzio hivyo kufanya iwe vigumu kuzuia wanafunzi kutoka nje ya shule pamoja na kufanya watu wasiokuwa na nia njema kuingia shuleni bila kuzuizi.
“Kutokana na changamoto hizo tunaomba wadau mbalimbali watusaidie ili tuweze kuzitatua na kuweza kuongeza kiwango cha ufaulu hapa shuleni na hatimaye kuweza kuwa shule ya mfano. “amesema.
Hata hivyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo na hivyo nchi kuendelea kuwa na mafanikio makubwa.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo,Obedi Melami amewataka wazazi kushirikiana pamoja na walimu katika kufuatilia mienendo ya watoto wao mashuleni badala ya kuwaachia jukumu hilo walimu peke yao kwani suala la kufuatilia maadili ni la kila mmoja wetu.