NJOMBE
Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake mkoa wa Njombe Scolastica Kevela amewataka akina mama kujianda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi za serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025 kwasababu wamethibitisha kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza kupitia kwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan.
Rai hiyo ameitoa katika kijiji mkutano wa hadhara katika kijiji cha Matola kilichopo halmashauri ya mji wa Njombe wakati wa ziara ya kamati ya siasa mkoa wa Njombe ikiongozwa na mjumbe wa halmashauri kuu Taifa mkoa wa Njombe(MNEC) Daniel Okoka ilipo tembelea na kisha kukagua miradi ya maendeleo katika Shule ya sekondari Matola ambako mradi wa Bweni na Nyumba ya mwalimu unatekelezwa ambapo Mama Kevela amesema wakati umefika kuchuana kwa hoja na akina baba jukwaani ili kufikia lengo la sera ya 50 kwa 50 katika uongozi hapa nchini.
Licha ya kuwataka akina mama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi lakini pia amewataka kutosahau majukumu yao ya ulezi wa familia na kisha kutoa rai kwa akina baba kuhakikisha wanaongeza upendo kwa akina mama ikiwa ni pamoja na kuwaunga mkono katika jitihada zao badala ya kuwakwamisha.
“Mtoto mbaya ni mtoto wa mama na mtoto mwenye akili na maadili ni wa baba hivyo akina mama tunapaswa kuzingatia jukumu letu la malezi yenye maadili ya watoto ili kusitokee kizazi kisicho na maadili kilichokengeuka,alisema Kevela mwenyekiti wa UWT Njombe
Awali Daniel Okoka ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu taifa mkoa wa Njombe akizungumza na wakazi wa Matola baada ya kukagua mradi wa nyumba ya mwalimu na bweni la wasichana shule ya sekondari Matola amesema kamati imeridhishwa na ubora wa miradi hiyo iliyogharimu fedha nyingi ya serikali na kisha kudai kwamba chama kitaendelea kufatilia na kufanya ukaguzi wa miradi yote inayotekelezwa kupitia ilani ya chama cha mapinduzi ili kusitokee ubadhirifu wa aina yoyote.
Katika hatua nyingine Okoka amezungumzia suala la Pembejeo kuwahishwa katika vituo vilivyochaguliwa ili wakulima wapate kwa wakati na kuendelea na msimu mpya wa kilimo kwasababu mkoa wa Njombe ambao ni lango kuu la uchumi umekuwa ndiyo ghara la taifa la chakula huku pia akiwahimiza wananchi kulima kwa wingi zao la parachichi kwakuwa lina soko la uhakika duniani kote.
Aidha MNEC huyo amewataka wakazi wanaopitiwa na mradi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami wenye thamani ya bil 95 kuanzia Itoni Njombe hadi Lusitu Ludewa kuchangamkia fursa ya kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kulisha maelfu ya watu wanaotarajiwa kuja kwenye machimbo ya mkaa wa mawe na chuma katika migodi ya Liganga na Mchuchuma.
Josaya Luoga ambaye ni katibu wa siasa na Uenezi mkoa wa Njombe katika mkutano huo wa hadhara ameonyesha kufurahishwa na kitendo cha wakazi wa kata ya Matola kuchangia katika miradi ya maendeleo kwa kujenga mabomba na kisha serikali kumaliza na kisha kuwa kuwataka kuendelea kufatilia kwa karibu kila mradi unaotekelezwa na kuhoji maendeleo yake ili utekelezaji ufanyike kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wao wananchi akiwemo Valelius Mwalongo na Jastin Ngailo wametumia mkutano huo kueleza changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kata yao ikiwemo changomoto ya maji ,upungufu wa walimu na huduma duni za afya na kisha kuomba chama cha mapinduzi kuona namna ya kuwasaidia kupata huduma hizo kama watanzania wengine.