Na Sophia Kingimali
Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA)kwa kushirikiana na Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kupitia tafiti zilizofanywa wamesaidia nchi kuwa ya tatu katika nchi zilizopo jangwa la Sahara ambapo watafiti 95 wamefaidika katika tafiti na mafunzo kupitia ufadhili wa (SIDA).
Akizungumza Oktoba 2, 2023 jijini Dar es salaam wakati wa kuadhimisha miaka 47 ya ushirikiano kati ya MUHAS na Sweden kupitia SIDA na miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden
Makamu Mkuu wa Chuo, MUHAS Profesa Aporinary Kamuhabwa amesema ushirikiano wao umekua wenye tija kubwa kwani wanafunzi wa uzamivu 95 wamefaidika.
Profesa Kamuhabwa amesema, walianzisha ushirikiano huo kwa lengo la kusaidia tafiti na mafunzo kama VVU/UKIMWI, kifua kikuu na malaria na kuongeza kuwa tafiti hizo zilichangia kuwepo kwa sera ya nchi.
“Sisi kama Chuo Kikuu cha Afya tafiti zetu na mafunzo yetu ziko kwa upande wa Afya na Sayansi Shirikishi, watafiti hawa wamesoma kwa njia za kufanya tafiti hivyo kupitia Sida tumefanya tafiti nyingi zikiwemo za magonjwa ya kuambukiza ambapo mwanzoni tulianza na ukimwi, kifua kikuu na malaria na magonjwa mengine”.
Amesema siku hizi magonjwa yanazidi kubadirika, na kuna magonjwa yasiyo ya kuambukiza hivyo mpango unaoendelea sasa ni kufanya tafiti katika magonjwa yasiyoambukiza na kuja na matokeo chanya.
“Chuo cha MUHAS ni Chuo cha tatu kwa ukubwa katika nchi ziliopo chini ya Jangwa la Sahara, hivyo mnaweza mkaona ushirikiano kama huu unafanya chuo kuweza kutambulika Kimataifa lakini tafiti ambazo zimefanyika kwa kushirikiana na MUHAS zimeweza kutoa majibu yanayolenga kutatua matatizo na changamoto za wananchi” amesema Kamuhabwa
Profesa Kamuhabwa ameongeza kuwa, ushirikiano huo pia umeiwezesha MUHAS kupata, teknolojia mpya zaidi ambalo tafiti zake zimechangia sana mabadiliko ya dawa haswa zile za malaria.
“Wakati wa Covid-19, MUHAS ilifanya utafiti juu ya chanjo, dawa na kinga”amesema
Ameongeza kuwa, mpango ulikuwepo wa mashirikiano kati ya Sida na MUHAS wa 2015 unaenda kufikia ukingoni na wanatarajia kuingia makubaliano mapya ambayo yanatarijiwa kusainiwa Novemba mwaka huu.
Amesema mpango huo utakaodumu hadi mwaka 2026 na utakuwa ni muendelezo wa kuendelea kutoa mafunzo kwa wanataaluma kwa ajili ya kufanya tafiti.
Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania Charlotta Macias mesema, Tanzania na Sweden zimeshirikiana kwa miaka 47 katika masuala ya VVU na Malaria na kwamba serikali yake kupitia SIDA imeisaidia MUHAS jumla ya dola za kimarekani bilioni 90 tangu kusainiwa kwa ushirikiano huo.
“Mafanikio makubwa yamepatikana hadi sasa na tunathibitisha hilo, ninatarajia kuona kwamba tunatia saini ya makubalino awamu mpya ya ushirikiano,” amesema
Naye Profesa Eligius Lyamuya wa Microbiology na Immunoology kutoka MUHAS amesema kuwa uwezo wa chuo kikuu kufanya utafiti umeongezeka.
Amesema SIDA imesaidia tafiti nyingi ambazo zimefanywa na kupelekea nchi kuwa nchi ya tatu Afrika katika tafiti ambapo awali SIDA ilikua inatoa fedha kwa ajili ya ugonjwa wa ukimwi lakini sasa inafadhiri mpaka magonjwa yasiyoambukiza.
Naye, Dkt. Mohamed Zahir, Mhadhiri wa MUHAS idara ya Micro Chemistry na Microbiology ambaye pia ni mnufaika wa mradi huo amewashukuru kamati iliyosoma mapendekezo yote yaliyoandaliwa na idara ya Chuo cha MUHAS.
” Mimi ni mmoja ya wanufaika wa fedha za kufanya tafiti kwahiyo malengo yangu yatatimia kwa kutengeneza miundombinu ili tuweze kuchukua damu kutoka mifumo ya uzazi na kutengeneza benki ya sampuli za seli na vinasaba ambavyo vitakuja kutusaidia au kuwatibu wagonjwa wa Selimundu.”
“Tunawashukuru SIDA na ubalozi wa Sweden kwa kutoa fedha ambazo zimetusaidia kama wanasayansi kukua kama mwanasayansi na kufanya tafiti ambayo Tanzania inastahili ili kuboresha miundombinu ya nchi katika sekta ya afya .” Ameongeza Dkt. Zahir
Pia amesema kwa sasa wanaweza kufanya tafiti zitakazo fanana na tafiti za nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Sambamba na hayo wakati wa maadhimisho Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Marcias amezindua maabara ya Biorepository na kituo cha ubunifu maeneo yote katika chuo cha MUHAS Mloganzila.