Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Biteko (katikati) akikata
utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha Nyanguku wilayani
Geita, Mkoa wa Geita. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine
Shigella.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa,
Wizara ya Nishati inafanya jitihada mbalimbali ili kupunguza makali ya
umeme nchini na hivyo kuwaondolea wananchi matatizo ya umeme
wanayoyapata kwa sasa.
Amesema hayo tarehe 02 Oktoba, 2023 baada ya kuwasha umeme katika
Kijiji cha Nyanguku na Bunegezi wilayani Geita, Mkoa wa Geita ambapo
pia alizungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali
ikiwemo ya maji na barabara katika vijiji hivyo.
“Tumekubaliana, Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi warudi
Dodoma kushughulia masuala ya mgawo wa umeme, tunataka tupunguze mgao
huu kwa kasi kubwa ili wananchi wasipate matatizo ya umeme, vilevile
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga anatembelea vituo vya kufua
umeme, alianzia Ubungo, ameenda Tegeta na maeneo mengine, lengo letu
ni lile, kupunguza makali ya mgawo wa umeme kwa watu wetu.”Amesema
Dkt. Doto Biteko
Ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati inalitekeleza agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la
kushughulikia changamoto za upatikanaji umeme wa uhakika ndani ya
miezi sita ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila matatizo.
Kuhusu umeme vijijini amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inataka
umeme uwafikie wananchi wote na kwa Mkoa wa Geita imetoa shilingi
bilioni 39 kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini mkoani humo na
dhamira ya Serikali ni kufikisha umeme kaya kwa kaya.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza suala la viongozi
kusimamia fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali, wawahudumie wananchi na kuwapa nyenzo za
kuwawezesha kufanya kazi ili wajikwamue katika maisha yao.
“Tunachotaka ni kuona kila senti iliyokusudiwa kwa ajili ya miradi
inawafikia wananchi, umetaka iwafikie, hutaki mwachie mwingine
anayetaka kuwahudumia wananchi, na nyie wananchi miradi ikijengwa
kwenye eneo lenu msiiache bali nendeni mkaisimamie kwani tunachotaka
kuona hii miradi inamilikiwa na wananchi.”amesisitiza Dkt. Biteko
Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), Mhandisi Jones Olotu, alisema kuwa, Mkoa wa Geita una 486 na
hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, REA imeshapeleka umeme kwenye
vijiji 359 na vijiji vilivyobaki tayari mkandarasi anaendelea na kazi
na ameshaanza kuwasha umeme kwenye vijiji alivyokabidhiwa.
Ameongeza kuwa, kwa Wilaya ya Geita Serikali imetoa shilingi Bilioni 2
ili kupeleka umeme kwa vijiji vilivyopo wilayani humo na shilingi
bilioni 6.9 zimetolewa kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vijiji-miji
vya wilaya ya Geita.