Na Prisca Libaga
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Majaliwa ameagiza Wizara ya malisili na utalii kupitia Bodi ya utalii kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kisiwa cha Mafia.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati akifunga Maonesho ya Utalii na Uchumi wa Bluu katika kisiwa cha Mafia.
Akitoa takwimu za idadi ya watalii waliokitembelea Kisiwa hicho tangu mwaka 2020 Waziri Mkuu amesema watalii 14,153 na walifika kisiwani Mafia na kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 2.7 na kuongeza kuwa mafanikio hayo ni juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini kupitia filamu ya The royal Tour.
Mhe. Majaliwa amesema azma yake ni kuona Kisiwa cha Mafia kikifunguka kwa utalii kama ilivyo Zanzibar na maeneo Mengine ya maarufu kwa utalii, na kuwataka wakazi wa Mafia wanatakiwa kuchangamkia fursa zitokanazo na utalii kisiwani humo.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa maliasili na Utalii Mhe. Dunstan KItandula alisema kuwa kisiwa cha Mafia kimebarikiwa kuwa na fukwe nzuri kwa ajili ya utalii ujulikanao kama utalii wa fukwe na pia eneo hilo lina utalii wa Papa Potwe ambao huvutia watalii kuja kutembelea kisiwa cha Mafia.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Wizara ya Malisili na Utalii kupitia bodi ya filamu itaendeleza jitihada za kutangaza vivutio vya utalii na kuibua mazao mapya ya utalii yanayopatikana katika kisiwa cha Mafia.