Mbunge wa Mlele Mhe. Isack Kamwelwe akifafanua jambo kwa wanakijiji wa Masigo wilayani Mlele wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua barabara ya Inyonga-Majimoto.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa wanakijiji wa Masigo wilayani Mlele wakati alipokagua barabara ya Inyonga-Majimoto.
Muonekano wa daraja la Kavuu linaunganisha miji ya Majimoto na Inyonga mkoani Katavi, daraja hilo linajengwa kutoa kuwa la vyuma hadi kuwa la zege ili kuwezesha magari makubwa kupita.
Muonekano wa barabara ya Kibaoni-Mlele junction KM 50 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Katavi.
……………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ametoa siku 7 kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Katavi kuja na ufumbuzi utakaowezesha kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kavuu linalounganisha mikoa ya Rukwa na Katavi kabla ya kuanza kunyesha kwa mvua za vuli.
Daraja la Kavuu lenye urefu wa mita 87.5 linajengwa tabaka la juu ili kuruhusu magari yenye uzito wa tani 56 kupita katika daraja hilo tofauti na awali ambapo liliruhusu magari yenye uzito wa tani 30 pekee.
“ Serikali imedhamiria kubadilisha tabaka la juu la daraja hili kutoka muundo wa nyuma (Marbey Logistic Support Bridge), kwa kujenga kwa kiwango cha zege (Reinforced Concrete Bridge), ili kuwezesha magari mengi makubwa kupita katika eneo hilo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao”, amesema Eng. Kasekenya.
Daraja la Kavuu linaunganisha miji ya Majimoto na Inyonga mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya barabara kuu ya ukanda wa mikoa ya kusini hadi magharibi inayoanzia Tunduma mkoani Songwe kupitia Sumbawanga, Namanyere, Majimoto, Inyonga, Mpanda, Uvinza, Kasulu hadi Nyakanazi mkoani Kagera.
Naibu Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa daraja hilo kukamilika kabla ya mzua za vuli ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza endapo daraja la muda litasombwa na maji ya mto Kavuu.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amemtaka mkandarasi M/s China Railway Seventh Group Co. Ltd (CRSG), anayejenga barabara ya Kibaoni-Sitalike sehemu ya Kibaoni-Mlele KM 50 kuongeza vifaa na wataalam ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati na ubora.
Amesisitiza nia ya Serikali ni kuufungua ukanda wa magharibi mwa nchi ili kuibua fursa nyingi za uvuvi, kilimo, biashara na utalii na hivyo kukuza uchumi.
Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi Eng. Abert Laiser amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa moja ya mradi unaokwenda kwa kasi mkoani humo ni ujenzi wa barabara ya Vikonge-Luhafwe KM 25 ambao ni sehemu ya barabara ya Mpanda-Uvinza -Kanyani KM 250.44 ambapo kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za uchukuzi kati ya mkoa wa Katavi na Kigoma.
Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ili kuona namna miundombinu ya barabara bora zitakavyo ufungua ukanda wa magharibi mwa Tanzania na kuwawezesha wananchi kuibua na kutumia fursa nyingi za kiuchumi katika ukanda huo.