Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuhakikisha wachimbaji wanapata masoko ya uhakika na kuwawezesha wawekezaji wadogo kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha.
Ameyasema hayo Septemba 30,2023 wakati wa kufunga Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita, amesema utafiti huo utasaidia kujua maeneo yenye madini ambapo aliwakilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman.
Amesema ili sekta ya madini iweze kuongeza mchango wale lazima ifungamanishwe na sekta nyingine kuwezesha taifa kupata maendeleo kwa haraka na upatikanaji wa ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
“Dira ya Sekta ya Madini (Vision 2030) itamaliza changamoto za muda mrefu kwa wachimbaji wadogo za kukosekana kwa taarifa za kuaminika za maeneo yenye rasilimali hiyo.
“Dira imelenga hadi kufikia 2030 utafiti wa madini kwa njia za jiofizikia uwe umefanyika nchini wa zaidi ya asilimia 50,” amesema Rais Samia.
Aidha ametoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iendelee kununua dhahabu ili nchi iweze kuwa na akiba ya kutosha.
Naye Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, amesema mahitaji makubwa ya wachimbaji ni teknolojia, mitaji na masoko ili kutengeneza ajira zaidi kwa Watanzania.
Mbunge wa Jimbo la Busanda, Tumaini Magesa ameishauri Serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji wachimbaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema mkoa huo ni wazalishaji wakubwa wa dhahabu ambapo imezalisha kilo 47,000 na kati ya hizo 36,000 zimezalishwa na wachimbaji wakubwa na 11,000 wachimbaji wadogo.
Amesema leseni 2,411 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na zingine 300 watakabidhiwa hivi karibuni.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini ndiyo inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni na kwamba kwa mwaka 2022/2023 iliingiza zaidi ya Dola bilioni 3.3 sawa na zaidi ya Sh trilioni 7.
“Tunaamini ifikapo mwaka 2025 mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa utafikia asilimia 10 kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” amesema Mavunde.