Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga Leo Septemba 29, 2023 akiwa katika ziara ya kukagua Kituo cha Kufua Umeme Ubungo II kilichopo Jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Kituo Cha Kuzalisha Umeme Ubungo II, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Deogratius Mulokozi (wapili kulia) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara ya kukagua Kituo Cha Kuzalisha Umeme Ubungo II.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kukagua Kituo Cha Kuzalisha Umeme Ubungo II.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (katikati), akikagua baadhi ya mitambo katika Kituo cha Ubungo II wakati wa ziara yake leo Septemba 29, 2023 jijini Dar es salaam.
Baadhi ya mashine za kuzalisha umeme katika Kituo cha Kuzalisha Umeme Ubungo II.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wizara ya Nishati imesema itahakikisha wanasimamia na kufatilia kila hatua utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuhakikisha linatekeleza majukumu kwa ufanisi ikiwemo matengenezo ya mashine za kuzalisha umeme ambazo zimeharibu na kusababisha uwepo wa mgao wa umeme.
Akizungumza leo Septemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akikagua Kituo cha Kufua Umeme Ubungo II, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema kuwa katika Kituo cha Ubungo I kuna mashine 12 za kuzalisha umeme lakini sita zipo katika matengenezo.
Mhe. Kapinga amesema kuwa maelekezo ya Wizara ni kuhakikisha TANESCO wanaweka mipango madhubuti ya kufanya marekebisho ya muda mfupi, kati na mrefu ili kufikia malengo ya watanzania kupata huduma ya umeme.
“Maelekezo ya muda mfupi yanapaswa kufanyika kwa muda mfupi na kwa wakati, mipango madhubuti ya matengenezo yanapaswa kufanyika kwa muda uliokusudiwa ili kuleta tija” amesema Mhe. Kapinga.
Amesema kuwa mashine kila mashine moja zilizoharibika zinauwezo wa kuzalisha megawatt 43, huku akieleza kuwa tayari mafundi wanaendelea na matengenezo.
“Ukiwa na mashine moja ambayo haifanyi kazi ya megawatt 43 ni umeme mwingi, lakini mafundi wanaendelea na matengenezo” amesema Mhe. Kapinga.
Katika hatua nyengine Mhe. Kapinga ametoa maagizo kwa TANESCO kuhakikisha ndani ya saa 6 yajayo Kituo kinarudi katika uzalishaji wa umeme pamoja na kutafute njia mbadala ili watanzania wapate huduma ya umeme.
“Sisi kama Wizara tutahakikisha tunawasimamia vizuri na kuwafatilia kila hatua ili mashine zifanyiwa marekebisho na kukamilika kwa wakati” amesema Mhe. Kapinga.
Amebainisha kuwa tayari Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suruhu Hassani ametoa maelekezo ndani ya miezi sita matengenezo yote yawe yamekamilika hivyo jukumu letu ni kusimama yote yanatekeleza kwa vitendo.