Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu Mb), akiwa na Mkurugenzi wa Miradi wa Mfuko wa Maendeleo wa Sweden (SWED FUND) Bw. Stefan Falk, walipokutana mjini Stockholm, Sweden, ambapo ameuomba Mfuko wa MMfuko huo kuweka kipaumbele cha kuisaidia Tanzania kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kukuza ajira na uchumi wa nchi kwa ujumla katika kuendelea kutekeleza dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,ya kuwaletea wananchi wake maendeleo kwa haraka, watakapo andaa Mpango Mkakati mpya wa Miaka Mitano wa Taasisi hiyo, mwakani (2024)
…………………………
Na Benny Mwaipaja, Stockholm, Sweden
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameuomba Mfuko wa Maendeleo wa Sweden (SWEDFUND) kuweka kipaumbele cha kuisaidia Tanzania kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kukuza ajira na uchumi wa nchi kwa ujumla katika kuendelea kutekeleza dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,ya kuwaletea wananchi wake maendeleo kwa haraka
Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo mjini Stockholm, Sweden, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Miradi wa SWEDFUND, Bw. Stefan Falk, ambapo walijadili masuala mtambuka ya ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Alisema kuwa Sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, utalii na sekta ya madini, zinaajiri watanzania wengi hususan vijana ambapo Serikali imeamua kuelekeza rasilimali kubwa kupitia Bajeti na program mbalimbali kukuza sekta hizo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa wakati SwedFund ikiandaa mkakati wake mpya wa maendeleo wa miaka mitano mapema mwakani, ni muhimu kuangalia namna Mfuko huo utakavyochangia katika mipango hiyo ya Serikali kwa kuwa licha ya kuongeza ajira kwa kundi kubwa la wananchi, lakini pia itaongeza uzalishaji wa mazao yatakayo liingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
Alisema mpango huo uweke bayana namna ya kuwekeza katika kuongeza tija katika sekta hizo kupitia teknolojia muhimu za kuongeza thamani ya mazao pamoja na namna ya kuyafikia masoko ya uhakika.
Dkt. Nchemba alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa kuchangia maendeleo katika kipindi cha miaka 60 ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, zikiwemo kilimo, afya, nishati, ujenzi wa miundombinu pamoja na kusaidia kupambana na umasikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi wa SwedFund, Bw. Stefan Falk, alisema kuwa uhusiano wa Tanzania na Sweden ni wa kupigiwa mfano na kwamba nchi yake iko tayari kuyafanyiakazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na Mhe. Dkt. Nchemba, kwa kuwa Sekta hizo ni muhimu katika kukuza uchumi wan chi na kupiga vita Umasikini katika jamii.
Aidha, alishangazwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi yanayotokea nchini Tanzania katika kipindi kifupi kilichopita licha ya changamoto zinazoikumba dunia hivi sasa na kutaka Sweden ijifunze kutoka Tanzania namna ilivyofanikiwa kudhibiti misukosuko ya kiuchumi pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za Maisha.
Dkt. Nchemba amemaliza ziara yake nchini Sweden ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Wizara za Kimkakati pamoja na mashirika na Taasisi za Fedha za Sweden ambapo pande hizo mbili zimekubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa faida ya pande zote mbili.