Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan ameungana
na mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi zinazozalisha kahawa duniani,
kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023
Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) iliyofanyika jijini
Tokyo, Japan tarehe 27 Septemba 2023.
Uzinduzi huo umeenda sanjari na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Maonesho
hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003.
Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yameandaliwa na Taasisi ya
Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ) na kushirikisha
makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi
zinazozalisha kahawa duniani. Maonesho haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29
Septemba 2023; na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji,
wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo.
Tanzania inawakilishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee
Board) ambayo, imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama vya ushirika na
makampuni ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na ufungashaji
wa kahawa yakiwemo, Kagera Cooperative Union (KCU), Kampuni
ya Kaderes Peasants Development (KPD), Kampuni ya Kamal Agro, Kampuni ya TANJA,
Kampuni ya Ubumwe na Kampuni ya Interbulk Packaging.
Aidha, katika maonesho hayo, Tanzania ina banda maalum la kuonesha
bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania, zinajumuisha kahawa iliyochakatwa
katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Pia, kupitia
maonesho hayo inaoneshwa na kutangazwa kahawa iliyo tayari kwa ajili ya
matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda
vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza, Afri Café na
Tanica.
Vilevile, siku ya pili ya maonesho hayo tarehe 28 Septemba 2023, Tanzania itapata fursa ya kufanya semina
maalum kuhusu kahawa ya Tanzania itakayoambatana na zoezi la uonjaji wa sampuli
za kahawa za Tanzania (Tanzania Coffee Seminar and Cupping Session) kwa
makampuni yapatayo 80 ya ukaangaji (coffee roasters) na usafirishaji kahawa ya
nchini Japan. Katika tukio hilo, sampuli za kahawa za wazalishaji na makampuni
ya Tanzania yapatayo 30 zitaoneshwa, kutangazwa na kuonjwa kwenye siku hiyo
iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini
(full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta.
Maonesho haya, ni fursa adhimu katika kukuza
soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina
maarufu la kibiashara la “Tanzania
Kilimanjaro Coffee”. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa
zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima
Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa
bora aina ya Arabica (Arabica laini – full washed na Arabica ngumu – natural)
inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro,
Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya
Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
Uzinduzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) |
Washiriki wakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) |
Washiriki wakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) |