Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akisalimiana na watendaji mbalimbali wa Serikali wajitokeza kumpokea wakatika akiwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (katikati) akiwasili katika eneo linalotarajia kujengwa Makao Makuu ya Kituo cha Uratibu wa Utafutaji wa Uokozi katika Ziwa Victoria (Maritime Rescue Coordination Centre – MRCC) jijini Mwanza
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akiwa katika ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira Pasiansi jijini Mwanza
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akijadili jambo na watendaji mbalimbali wa Serikali walipotembelea eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Kituo cha Uratibu wa Utafutaji wa Uokozi katika Ziwa Victori
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifuatilia maelezo kutoka kwa Kaptain Kwila Nkwama alipotembelea mradi wa ukarabati wa Meli ya Utafiti ya Jumuiya (RV Jumuiya)
………………………….
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.) anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki amewataka watendaji na wasimamizi wanaosimamia utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali katika jiji la Mwanza kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (Lake Victoria Basin Commission –LVBC) kuhakikisha inatelezwa kwa kasi na ufanisi ili iwanufaishe wananchi wenye uhitaji.
Naibu Waziri Byabato amebainisha hayo wakati akiendelea na ziara ya kikazi ya ukaguzi wa ufanisi wa programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa kupitia LVBC.
“Nitoe rai kwenu watendaji na wasimamizi wote wa miradi hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa katika Kanda ya Ziwa kupitia LVBC kuhakikisha sote kwa umoja wetu tunafanya kazi usiku na mchana kutimiza adhma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuona Wananchi wa Tanzania wananufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na Jumuiya kijamii na kiuchumi”.alisema Mhe. Byabato
Akiwa jijini Mwanza tarehe 26 Septemba 2023 Naibu Waziri Byabato ametembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira chini ya programu ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa Rasilimali za Maji (Lake Victoria Basin Integrated Water Resources Management Programme LVB – IWRMP) katika eneo la Pasiansi. Progamu hii inalenga kuchangia katika usimamizi endelevu wa rasilimali za maji ya Ziwa Victoria ili kuongeza ubora na upatikanaji wake kwa matumizi mbalimbali, ikihusisha usambazaji wa majisafi kwa kaya zilizopo maeneo ya milimani na ujenzi wa miundombinu ya majitaka na vyoo vya kisasa. Maeneo mengine yanayotarajia kunufaika na programu hiyo katika Jiji la Mwanza ni pamoja na Kitangiri, Mabatini, Kirumba na Nyamanoro.
Sanjari na hayo kupitia utekelezaji wa mradi huu wa kupanua miundombinu ya majitaka katika Jiji la Mwanza wenye thamani ya shilingi bilioni 12.7 kutaweizesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kukarabati na kupanua mtandao wake wa majitaka kwa takriban 14.4km na kuunganisha kaya 1,600 kwenye mtandao huo.
Programu na Miradi mingine aliyozitembelea Mhe. Byabato jijini Mwanza ni pamoja na; ujenzi wa Makao Makuu ya Kituo cha Uratibu wa Utafutaji wa Uokozi katika Ziwa Victoria (Maritime Rescue Coordination Centre – MRCC), Ukarabati wa Meli ya Utafiti ya Jumuiya (RV Jumuiya) iliyopo Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza Kusini unaofanywa na Kampuni ya kitanzania ya Mundao Engineering na eneo la Machinjio lililopo eneo la Nyakato ikiwa ni sehemu ya Programu ya Usimamizi wa Mazingira katika Ziwa Victoria
Katika hatua nyingine Wananchi wa Pasiansi kwa nyakati tofauti wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuvutia utekelezaji wa mradi wa kupanua miundombinu ya majitaka katika Jiji la Mwanza ambao wameutaja kuleta mageuzi makubwa katika utunzaji wa mazingira na upatikanaji wa maji safi.
“Hapo mwanzoni kabla ya kufikiwa na mradi huu sisi tunaoishi maeneo ya huku chini ya mlima tulikuwa tunaathiriwa sana na uchafu kutoka kwa wenzetu wanaoishi huko mlimani, tunaishukuru sana Serikali kwa kutekeleza mradi huu ambao umemaliza kabisa tatizo hilo, kwa sababu kila kaya imepata choo bora sambasamba na mifumo ya majitaka iliyo imara”. Alieleza Mzee William Mchomvu mkazi wa Pasiansi.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Naibu Waziri Byabato toka ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Naibu Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Katika ziara hiyo Naibu Waziri Byabato ameambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria yenye Makao Makuu yake mjini Kisumu, Kenya ilianzishwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Itifaki iliyosainiwa tarehe 29 Novemba, 2003. Jukumu la Kamisheni hiyo ni kuratibu usimamizi endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria ikiwemo utekelezaji wa Miradi ya Mazingira, Miundombinu ya Kiuchumi na Kijamii katika Bonde la Ziwa Victoria kwa manufaa ya Nchi Wanachama hususan zinazopakana katika Bonde hilo ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Uganda.
Kamisheni hii inaongozwa na Katibu Mtendaji ambapo kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Dkt. Masinde Bwire kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.