Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Mitawi akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo kwa Maafisa ununuzi wa Wizara za Serikali ya MaPinduzi Zanzibar kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal leo Jumanne Septemba 26, 2026, Zanzibar. Kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Bi Farhia Ali Mbarouk na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na (Mazingira) Mhandisi Catherine Bamwenzaki.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Mitawi akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo kwa Maafisa ununuzi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal leo Jumanne Septemba 26, 2026, Zanzibar. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Catherine Bamwenzaki.(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
….
Na Mwandishi Wetu, OMR- ZANZIBAR 26/9/2023.
MAAFISA Ununuzi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo wakati wa ununuzi wa vifaa na vitendea kazi vyenye kemikali zilizowekewa ukomo wa matumizi ili kuzuia athari uharibifu wa mazingira na kulinda afya za binadamu.
Rai hiyo imetolewa leo Jumanne (Septemba 26, 2023) hapa Zanzibar na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdalllah Mitawi wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa Maafisa Ununuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.
Kwa mujibu wa Mitawi amesema asilimia kubwa ya bajeti ya Serikali imeelekezwa katika eneo la ununuzi wa vifaa na vitendea kazi mbalimbali katika ofisi za umma, hivyo ni wajibu wa maafisa manunuzi kuhakikisha wanazingatia miongozo iliyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ili kuepusha hasara kwa serikali na kulinda afya kwa binadamu na mazingira.
“Maofisi yote ya umma tunatumia viyoyozi na majokozi kama sehemu ya kupata hewa safi…Maafisa ununuzi ndio mnahusika moja kwa moja katika ununuzi wa vitendea kazi hivi…Tunapaswa kufahamu kuwa kunaaina fulani ya kemikali zilizopo katika vitendea kazi hivi zina athari kwa mazingira yetu….kupitia mafunzo haya mtaweza kufahamishwa” amesema Mitawi.
Mitawi amesema kwa mujibu kwa Itifaki ya Montreal ambapo Tanzania iliridhia mkataba huo mwaka 1993, nchi zote 197 zimekubaliana kutotumia kemikali zilizodhibitiwa kupitia ili kulinda Tabaka la ozoni kwa kuwa hatua hiyo itasaidia juhudi za ulimwengu kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto, ukame na vifo vya binadamu, wanyama na mifugo.
Akifafanua zaidi Mitawi amesema maafisa ununuzi na ugavi wana nafasi kubwa ya kuisadia Serikali na jamii kwa ujumla kuhusu udhibiti wa kemikali zilizodhibitiwa kwa mujibu wa itifaki ya Montreal ambapo kwa kutambua umuhimu huo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa imeendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa wa kada hiyo.“Baada ya mafunzo haya mtapokuwa maofisi…Hakikisheni pale ambapo Katibu Mkuu au Afisa Masuhuli akihitaji kufanya manunuzi ya viyoyozi au majokofu…ni wajibu wenu kuhakikisha tunatoa ushauri wa kitaalamu kama ambavyo tutaelekezwa na wakufunzi kupitia mafunzo haya” amesema Mitawi.
Mitawi amesema dunia kwa sasa imeshuhudia kiwango kikubwa cha athari za mabadiliko ya tabia ikiwemo ongezeko la joto katika maeneo mbalimbali, magonjwa, mvua zisizotabirika na ukame uliokithiri unaotokana matendo unaofanywa na binadamu ikiwemo uharibifu wa tabaka la ozoni.
“Sote ni mashahidi kwa yanayotokea kwa sasa huko Ulaya….Tunaelezwa na wanahistoria kuwa dunia imekabiliwa na kiwango kikubwa cha joto kuwahi kutokea…..Mafunzo yana umuhimu mkubwa kwetu katika kutambua aina ya vifaa vyenye kemikali vinavyonunuliwa katika Ofisi zetu vimezingatia Itifaki ya Montreal ili kunusuru afya za binadamu na mazingira” amesema Mitawi.
Mitawi amesema Tanzania kama nchi imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana athari za mabadiliko ya tabianchi yenye lengo la kudhibiti uingizaji na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kushirikiana na ili kuzuia madhara mbalimbali kwa jamii ikiwemo magonjwa, ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Catherine Bamwenzaki amesema asilimia kubwa ya kemikali zinazoharibu tabaka la ozone zimekuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi, hivyo ili kujenga uelewa wa pamoja Serikali imeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii.
“Asilimia kubwa ya kemikali hizi tumekuwa tukizinunua kutoka nje ya nchi…hivyo tukiwa kama Maafisa Ununuzi tunapaswa kuwa mstari wa mbele tunatoa ushauri wa kitaalamu na elekezi katika ununuzi wa vifaa na vitendea kazi ili uharibifu wa tabaka la ozoni” amesema Mhandisi Bamwenzaki.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Bi Farhia Ali Mbarouk ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yataongeza tija na ufanisi kwa Maafisa ununuzi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Mafunzo kwa maafisa ununuzi wa Wizara za SMZ zitaongeza tija kwa watendaji wetu katika katika kutambua vifaa na vitendea kazi vyenye kemikali zenye ukomo wa matumizi” amesema Farhia.