Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Deogratius Balile akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Daudi Kosuna akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii(NSSF), Lulu Mengele akitoa neno la utangulizi katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.
Menejimenti kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakiwa katika Mkutano na Wahariri wa vyombo vya Habari.
Wahariri wa Vyombo vya Habari wakichangia mada katika kikao kazi na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
……
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefanikiwa kuongeza makusanyo ya michango kutoka shilingi bilioni 97.67 hadi kufikia bilioni 143.05 katika kipindi Cha kuanzia Marchi 1, 2021 hadi mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari katika kikao kazi kilichofanyika leo Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba, amesema kuwa ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaoleta michango kwa wakati na mazingira ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi.
Bw. Mshomba amesema kuwa makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia shilingi bilioni 1,718.28 katika mwaka ulioishia Juni 30, 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 1,201.05 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2021.
Amesema kuwa pia wanachama wachangiaji katika mfuko wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia Juni 30, 2023 wanachama wachangiaji walikuwa 1,189,222 ukilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa kwa Juni 30, 2021.
Amefafanua kuwa pia wamefanikiwa kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuleta tija kwa Taifa.
“Uwekezaji wa Mfuko (investment portfolio) iliongezeka kwa asilimia 111 kutoka shilingi bilioni 3,395.46 Machi 1, 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 Juni 30, 2023 ikichangiwa na kukua kwa thamani ya vitega uchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.” amesema Bw. Mshomba.
Amesema kuwa thamani ya vitega uchumi vya mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 Juni 30, 2023 kutoka shilingi bilioni 4,622.25 zilizofikiwa Juni 30, 2021.
Mshomba ameeleza kuwa wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023, yalifika shilingi bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na shilingi bilioni 37.35 zilizokusanywa mwezi Machi 2021.
Amesema kuwa mapato halisi (real rate of return on investment) ya mfuko, amesema yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 mwezi Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia Juni 30, 2023.
“Mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia shilingi bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha Juni 30, 2021.” amesema Bw. Mshomba.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023, mfuko ulilipa shilingi bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ukilinganisha na shilingi bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia tarehe Machi 1, 2021.
“Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) na mkupuo maalum (special lumpsum).” amesema Bw. Mshomba.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia shilingi bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2021.
NSSF ulianzishwa mwaka 1964 kama kitengo ndani ya Wizara ya Kazi kinachoshughulikia mafao ya wafanyakazi baada ya kustaafu. Mwaka 1975, kitengo hicho kiliboreshwa na kuwa taasisi inayojitegemea iliyoitwa National Provident Fund (NPF).
Maboresho zaidi yalifanyika mwaka 1997, ambapo Sheria Na. 28 ilitungwa na kuibadili NPF kuwa Mfuko wa Pensheni, hivyo kuwezesha kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi.
Mwaka 2018 Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii yaliyosababisha kurekebishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50.
Uamuzi huo uliifanya NSSF kuwa mfuko pekee unaohudumia hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na wale wa sekta isiyo rasmi nchini.