Na Lilian Lundo – MAELEZO
Wananchi wa Kijiji cha Ihako kilichopo Kata ya Katome, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha kupatikana kwa umeme kijijini hapo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Pongezi hizo zimetolewa leo Septemba 24, 2023 siku mbili kabla ya kuwashwa kwa umeme wa REA kijijini hapo, ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko anatarajiea kuwasha umeme kijijini hapo.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutukumbuka, maana kijiji hiki kiliachwa nyuma kwa muda mrefu, kuna baadhi ya huduma tulikuwa tunakosa kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika,”amesema Ramadhani Mabula mkazi wa Ihako
Ameendelea kusema kuwa, mara baada ya umeme kuashwa kijijini hapo, anatarajia kufungua sehemu ya kurekodi miziki pamoja na kuuza vinywaji baridi, biashara ambayo alishindwa kuifanya kwa muda mrefu kutokana na kutowepo kwa umeme kijijini hapo.
“Kutokana na shughuli yangu ya ufundi kinyozi, nilikuwa nikipata changamoto nyingi Kupitia umeme wa sola ambao nilikuwa nikitumia, mfano kipindi cha mvua nilikuwa nashindwa kufanya biashara kutokana na sola inategemea jua, ili iweze kufanya kazi,” amesema Makelele Mabula mkazi wa kijijini hapo.
Amesema kuwa, kuwashwa kwa umeme wa REA kijijini hapo kutamsaidia kufanya kazi ya ukinyozi kipindi chote cha jua au mvua, kwani umeme huo ni wa uhakika zaidi ukilinganisha umeme wa sola ambao walikuwa wakiutumia.
Naye Mfanyabiashara wa duka la dawa baridi, Sophia Nyanda ameipongeza REA kwa kuwafikishia umeme kijijini hapo, hivyo kumuwezesha kununua jokofu la kutunzia dawa ambazo zinahitaji kuhifadhiwa kwenye baridi.
“Kuna baadhi ya dawa nilikuwa nashindwa kuuza kutokana na kutokuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme, lakini kuwashwa kwa umeme wa REA katika kijiji chetu, kutawezesha kutumia jokofu kwa ajili ya kuhifadhia dawa zinazohitaji baridi,” amesema Sophia.