Na. Zillipa Joseph, Kata
Mpaka kukamilika kwa siku nne za chanjo ya polio II ya nyumba kwa nyumba; mkoa wa Katavi unatarajia kufikia jumla ya watoto 227,862 wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi miaka nane.
Chanjo hii ambayo itafanyika katika mikoa sita iliyo mipakani na nchi za jirani inakuja baada ya mtoto mmoja wa Sumbawanga Vijijini katika mkoa wa Rukwa kubainika kuwa na ugonjwa wa polio kirusi namba mbili.
Hali hii inajitokeza kutokana na mwingiliano na nchi za Malawi, Msumbiji Kongo DRC, na Burundi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo za kibiashara.
Kwa mujibu wa Mratibu wa chanjo mkoa wa Katavi bwana Kahindi Stephan, chanjo nchini Tanzania zilianza kutolewa mwaka 1975 ambapo kulikuwa na chanjo tatu tu, na mpaka sasa Tanzania ina jumla ya chanjo kumi zenye uwezo wa kukinga magonjwa 14.
Bwana Kahindi aliyataja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kifua kikuu, polio, nimonia, ugonjwa wa kuhara(rotavac), surua, na rubella.
Mengine ni dondakoo, uti wa mgongo, kifaduro, pepopunda, homa ya uti wa mgongo na homa ya ini; tetanus, saratani ya mlango wa kizazi na virusi vya korona.
Aliongeza kuwa ugonjwa wa polio kwa mara ya mwisho tanzania ulijitokeza mwezi Julai mwaka 1996 katika mkoa wa Mtwara.
Aidha, ametaja sababu za kuanza upya kwa kampeni ya chanjo ya polio II kufuatia mtoto mmoja wa mkoani Rukwa kubainika kuwa na virusi vya polio II kwani mwaka 2016 Shirika la Afya duniani (WHO) lilisitisha chanjo ya polio II baada ya kujiridhisha kuwa ugonjwa huo umekwisha mwaka 2015.
Akielezea sababu za kuchanja watoto wa umri wa miaka sifuri mpaka nane na sio miaka mitano kama ilivyozoeleka bwana Bahati Mwailafu ambaye ni Afisa Afya ngazi ya jamii kutoka Wizara ya Afya alisema kwa kipindi cha miaka nane iliyopita chanjo ya polio II ilisitishwa.
Mwailafu aliongeza kuwa kwa sasa chanjo ya polio iliyokuwa inaendelea kutolewa kwa watoto ni polio I na polio III.
Kwa upande wake daktari na mdau wa afya ya uzazi na watoto kupitia Wizara ya Afya dk. Keja Muruke alisema dhamira kuu ya chanjo ni watoto kupata kinga kamili.
‘Kuchanja ni salama zaidi kuliko kutokuchanja’ alisema dk. Muruke.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi Mratibu wa elimu ya afya kwa umma mkoa wa Katavi, Bi. Suzana Komba ameomba ushirikiano kwa waandishi wa habari katika kuielimisha jamii umuhimu wa chanjo.
Bi. Komba alisema jamii inapaswa kuelewa kuwa kanuni za msingi wa afya bora ni pamoja na usafi na kuitaka jamii kuondoa dhana potofu juu ya chanjo ili watoto wapate chanjo.
Katika kufuatilia uelewawa jamii kuhusu chanjo mwandishi wa habari hizi alipita katika baadhi ya mitaa na kuzungumza na watu mbalimbali.
Bi. Lucy Rocky ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa wiki saba, anakiri kutomrudisha mtoto wake hospitali baada ya kujifungua na pia haelewi ugonjwa wa polio ni ugonjwa wa aina gani.
Kwa mujibu wa Lucy anayekaa mtaa wa Shanwe katika manispaa ya Mpanda alisema anategemea kumpeleka kliniki mtoto wake atakapofikisha miezi miwili.
Naye Amina Abdallah mkazi wa Makanyagio mwenye mtoto wa mwezi mmoja anasema alijifungulia nyumbani baada ya kukosa hela ya vifaa vinavyohitajika hospitali wakati wa kujifungua.
Amina alisema bado anaogopa kumpeleka mtoto hospitali kwani kwani anahofia kupigwa faini ya kujifungulia nyumbani.
Alipoulizwa kuhusu chanjo ya polio alisema wakipita atawaruhusu wamchanje mwanae na kupendekeza chanjo zote ziwe zinapita nyumba kwa nyumba ili kuwanusuru wenye duni na waliozalia nyumbani kama yeye.
Chanjo ya polio kirusi namba II inaendelea kutolewa mkoani Katavi kupitia kampeni ya nyumba kwa nyumba kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba mwaka huu.