Na Sophia Kingimali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amewataka wakurugenzi wa majiji kusimamia miradi iliyopo kwenye majiji yao ili ikamilike kwa wakati kama mikataba ya miradi hiyo inavyosema ili kuondoa mianya ya rushwa.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam septemba 23 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji ya Tanzania(TACTIC) ambao utatekelezwa kwa miji 45 na utagharimu zaidi ya sh. trilioni moja.
“Katika eneo la fedha za miradi kumekuwepo na changamoto hata kwa TAMISEMI, ninakuagiza mkalifuatilie mara moja, wakati mwingine fedha zinatumwa katika halmashauri na majiji,’’ amesema
Ameongeza; “Baadhi ya Wakurugenzi wa majiji na baadhi ya watendaji TAMISEMI, sasa lazima na sisi tujiangalie wanaoshirikiana na mtandao.
“ Zinatumwa fedha takribani sh. milioni 500 kwa baadhi ya wakurugenzi zinatolewa fedha hizo na zote wanagawana, sasa hili ulifuatilie kwa sababu ninazo taarifa na ushahidi wa baadhi ya halmashauri tano ambazo wanaingiziwa fedha na zinatolewa kinyemela kisha kugawana,” amesema Mchengerwa
Pia amemuomba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni kuingilia kati suala hilo ili wanaohusika wote wachukuliwe hatua.
“Ninyi Wakurugenzi mmekasimiwa madaraka na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baadhi katika maeneo yenu zimepelekwa fedha za miradi na wengine hadi muda huu hazijaanza kutekeleza miradi husika, sasa usimamizi wa miradi hii, Katibu Mkuu isipokwenda vizuri sitajali ni nani amewekwa pale, nitamsimamisha kazi, nendeni mkachape kazi kuwasaidia Watanzania,” amesema.
Amesema, kwa Mkurugenzi ambaye ni mzembe anayeendekeza vitendo vya rushwa hatakuwa sehemu ya serikali inayoendeshwa na Rais Dk. Samia kwani katika kipindi chake hatakubali uzembe huo na hatakuwa na huruma zaidi ya kuchukua hatua.
“Mikataba tuliyoisaini imegharimu takribani dola za kimarekani milioni 410 zaidi yash. trilioni moja na utatekelezwa katika miji 45 na kwa awamu ya kwanza litajumuisha miji 12 ambayo ni jiji la Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Ilemela, Morogoro, Kahama, Kigoma Ujiji, Songea, Sumbawanga, Tabora na Geita,” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi ya Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, Mhandisi Hamphrey Kanyenye amesema utekelezaji wa maeneo hayo 12 utaanza katika mwaka huu wa fedha na mradi utagharimu kiasi cha sh. bilioni 276.18 ikihusisha gharama za usimamizi ambazo ni sh. bilioni 17.05.
Katika mikataba hiyo wanatarajia kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 147.54 kwa kiwango cha lami, madaraja, vivuko maji , taa za barabarani zenye mfumo wa kutumia umeme wa jua, njia za watembea kwa miguu na mitaro maji ya mvua hivyo amewata wakurugenzi kukamilisha miradi hiyo kwa muda ulipangwa.
Pia, wameanza kwa miji hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu, awamu ya pili itahusisha miji ya Babati, Bariadi, Bukoba, Iringa Kibaha, Korogwe, Lindi, Moshi, Mpanda, Mtwara, Musoma, , Njombe, Singida, Shinyanga na Tanga huku awamu ya tatu ikiwa ni Bagamoyo, Bunda, Chato, Handeni, Ifakara, Kasulu, Kondoa, Mafinga, Makambako, Masasi, Mbinga, Mbulu, Nanyamba, Newala, Nzega, Tarime, Tunduma na Vwawa.