Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa akitoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa wananchi wa Kata ya Bugogwa,Sangabuye,Shibula na Kayenze.
Elimu ya kuzuia uhalifu ikiendelea kwa wananchi wa Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza.
………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbrod Mutafungwa amewaonya watu wanaofanya uhalifu ndani ya Ziwa Victoria ikiwemo Uvuvi haramu huku akiahidi kwamba Jeshi la Polisi halitomvumilia mhalifu.
Kamanda Mutafungwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 23, 2023 wakati akitoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa wananchi wa Kata ya Bugogwa, Sangabuye, Shibula na Kayenze Wilayani Ilemela mkoani hapa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake yenye lengo la kutoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Kupitia kikao hicho Kamanda Mutafungwa ametangaza wakati mgumu kwa wahalifu wanaopora vyavu za wenzao na mazao ya uvuvi huku akiahidi hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya yao.
Amesema kuanzia leo msako mkali wa kuwasaka wahalifu katika maeneo yote unaendelea, watafute pa kwenda maana inakuja Opereseheni kali ambayo itawapa wakati mgumu sana wahalifu.
“Tunachoomba kutoka kwenu wananchi ni ushirikiano maana mpaka sasa tunamajina ya wahalifu na tutawafuata popote walipo iwe majini au nchi kavu” amesisitiza Mutafungwa.
Aidha, Kamanda Mutafungwa ameomba ushiriki wa jamii kutokomeza vitendo hivyo kwa kile alichosema usalama wa nchi unalindwa na kila mwananchi ili kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea nchini.
“Wote kwa pomoja tunatakiwa kuwatambua watu wabaya na kuwatolea taarifa, ninyi ni watanzania lazima muwe wazalendo kwa nchi yenu” amesisitiza Mutafungwa.
Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa amekemea vitendo vya imani za kishirikina ikiwemo Kamchape na Lambalamba na kuwataka wanaoendesha shughuli hizo kujisalimisha wenyewe kwa Jeshi la Polisi kabla hawajaanza kusakwa.