Na. Happiness Shayo, Dar – es – Salaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameipongeza Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) kwa kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuweza kuitunza nyumba ya utamaduni, kuwa na namna mbalimbali za maonesho na mikusanyo zaidi ya laki nne nchini.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea eneo la Makumbusho ya Taifa kwa lengo la kuangalia utendaji kazi wao.
“Tumefurahia kwa jinsi ambavyo Makumbusho ya Taifa wameweza kuitunza nyumba ya utamaduni na kuwa wabunifu kwa kuanzisha aina mbalimbali za maonesho na kuwa na mikusanyo zaidi ya laki nchini” alisema Mhe. Kairuki
Sanjari na hayo, Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watendaji wa Taasisi hiyo kuendelea kuwa wabunifu ikizingatiwa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepitisha muundo mpya kwa ajili ya taasisi hiyo.
Aidha, Mhe. Kairuki ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuboresha maeneo mapya hasa kwenye eneo la utafiti na kuhakikisha kwamba nafasi muhimu za rasilimaliwatu zinajazwa akitolea mfano nafasi za Maafisa Utamaduni na Maafisa Utalii.
Amesema lengo la kuendelea na maboresho mbalimbali katika Makumbusho ya Taifa ni kuvutia watalii wengi zaidi wanaokuja nchini na kuwafanya waweze kurudi kwa mara nyingine.
“Tunaangalia ni namna gani tutaweza kuvutia watalii waje nchini na wakija wasije mara moja, ni nini kitakachomvutia mtalii aje mwakani pia ndio maana tunaendelea kufanya ubunifu zaidi kuona ni namna gani kuwa na maonesho mengi ya aina mbalimbali ya kielimu, kiutamaduni na kiutalii katika makumbusho yetu pamoja na malikale” alisema Waziri Kairuki
Vilevile, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuangalia namna bora za kuboresha
malikale nchini na amewakaribisha watu binafsi kuanzisha makumbusho zao ili kuhakikisha mila, utamaduni na historia za Mtanzania zinatunzwa.
Ziara hiyo iliyolenga kuangalia uwajibikaji imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula (Mb) na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi pamoja na watendaji na watumishi wa Makumbusho ya Taifa.