………………..
Na Sixmund Begashe
Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kujiimarisha katika mikakati ya kupambana na Ujangili.
Katika azma hiyo, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) inatekeleza Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT) ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na UNDP.
Akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wa matumizi ya mfumo wa kubadilishana taarifa wa EAC TWIX maafisa intelijensia na himasheria Jijini Arusha kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Fortunata Msoffe amesema kuwa Wizara itaendelea kutanua wigo wa Kimataifa katika kupambana na Ujangili.
Dkt. Msofe amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Sukuhu Hassan kwa jitihada kubwa za kuinua utalii nchini hasa kupitia Filamu ya The Royal Tour, hivyo Wizara hiyo inaendelea kujihimarisha kuhakikisha maliasili nchini zinalindwa ili kuimarisha sekta ya utalii na uhifadhi.
Naye Mkurugenzi wa TRAFFIC Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Mikala Lauridsen ameishukrani Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa chini ya Mpango wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori nchini Tanzania kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili (IWT – Project) pamoja na kuwaalika TRAFFIC kutoa mafunzo katika warsha hiyo.
Aidha Meneja wa Mradi wa Kupapamba na Ujangili Bw. Theotimon Rwegasira amesema Mradi wa kupambana na ujangili umelenga kusaidia juhudi za Serikali za kutokomeza ujangili nchini.
Bw. Rwegasira ameongeza kuwa warsha hiyo ni mwendelezo wa kazi za Mradi wa IWT katika kujenga uwezo wa kitaasisi wa kupambana na ujangili, na utekelezaji wa Mkakati wa KItaifa wa kupambana na ujangili uliozinduliwa hivi karibuni.
Ameeleza pia kuwa katika vipengele vya Mradi, suala la kushrikiana kati ya Tanzania na nchi nyingine na jumuiya ya kimataifa limepewa kipaumbele ikiwemo, matumzi ya teknolojia, kubadilishana taarifa za kiintelijensia.