Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Arumeru,Noel Severe akiwa na kamati ya siasa wilaya ya Arumeru,akikagua madawati katika shule ya sekondari Oldadai iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Diwani wa kata ya sokon 11,Obedi Melami akielezea miradi mbalimbali katika kata yake wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Shule ya sekondari Sokon 11 ambayo ilitembelewa na kamati hiyo huku Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arumeru,Noel Severe akipongeza ujenzi wa shule hiyo na mazingira mazuri ya kuvutia.
Muonekano wa daraja linalounganisha kiutu na Sokon 11 ambalo shs 438 bilioni zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wake.
…….
Julieth Laizer, Arusha .
Arusha Viongozi wa ccm katika kata mbalimbali wilayani Arumeru kwa kushirikiana na watendaji wa kata wametakiwa kusimamia kwa karibu miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ili iweze kuwanufaisha wananchi na kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arumeru Noel Severe akiwa katika ziara na kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi wilaya ya Arumeru mkoani Arusha katika kukagua miradi ndani ya kata ya Sokon 11 kati ya kata 27 zinazotembelewa kwa ajili ya kukagua miradi hiyo.
Aidha Severe amesema kuwa ,serikali imekuwa ikitoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ila changamoto iliyopo ni baadhi ya viongozi kutosimamia kikamilifu miradi hiyo ili iweze kuwa kwenye viwango vinavyotakiwa.
“Tumetembelea miradi mbalimbali katika kata hii ikiwemo mradi wa bweni katika shule ya sekondari Oldadai, kituo cha afya cha Ng’iresi na jengo la utawala la shule hiyo ambapo tumebaini mapungufu mbalimbali ikiwemo kusuasua kwa miradi hiyo na kutotumia fedha za serikali ipasavyo na baadhi ya miradi kutekelezwa chini ya viwango jambo ambalo halitakiwi kabisa .”amesema.
Katika ziara hiyo pia kamati imepongeza kukamilika kwa mradi wa daraja na barabara ya Kiutu na Sokoni II ambayo hapo awali ilikuwa ni changamoto kubwa baada ya kusombwa na mafuriko na kusababisha kukosa mawasiliano baina ya kata hizo.
Aidha amewataka viongozi hao kuzionea huruma fedha hizo zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi badala ya kuinyamazia pindi wanapoona miradi hiyo inatekelezwa chini ya kiwango na kuendelea kuiletea serikali hasara kubwa.
Naye Diwani wa kata ya sokon 11 wilayani Arumeru,Obedi9 Melami amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anatoa fedha kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi ikiwemo katika kata hiyo ambayo imepewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja linalounganisha kata ya Kiutu -Sokon 11 baada ya daraja lililokuwepo kuzolewa na mafuriko makubwa ambapo ilitolewa kiasi cha shs 438 milioni na serikali kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
Melami amesema kuwa,ujenzi wa daraja hilo umeanza juni 6 mwaka huu ambapo kukamilika kwa daraja hilo kutaleta mafanikio makubwa kwa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha amewataka viongozi wa kata ccm na matawi kuhakikisha wanatembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ili iweze kufanyika kwa umakini mkubwa na thamani halisi ya fedha katika miradi hiyo iweze kuonekana.
“Namshukuru sana Rais Samia kwa namna ambayo ametusaidia katika kata yetu kwa kutoa fedha ya kutekeleza miradi mbalimbali ,na naomba sana Tarura wilaya ya Arumeru kuongeza bajeti kwa ajili ya kukamilisha miradi ya barabara ambayo bado ni changamoto hasa kipindi cha mvua kwani barabara nyingi zimekuwa hazipitiki kabisa.”amesema .
Nao baadhi ya wananchi walimpongeza Rais Samia kwa namna ambavyo anazidi kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo mbalimbali huku wakimwomba kuendelea kusaidia zaidi katika kata hiyo ya Sokon 11 hasa katika swala zima la barabara.